Kijiji cha Nyuki kinaendelea kuandika historia kwa kuimarisha nafasi yake katika soko la kimataifa kupitia uzalishaji wa bidhaa bora zinazotokana na nyuki pamoja na kupanua ushirikiano na mataifa mbalimbali duniani.
Akizungumza kuhusu mafanikio hayo, Mkurugenzi wa Kijiji cha Nyuki, Philemoni Kiemi, amesema taasisi hiyo imefanikiwa kufanya tafiti mbalimbali zilizowezesha kuongeza thamani ya mazao yanayotokana na nyuki na kuzalisha bidhaa nyingi zenye ubora wa hali ya juu zinazokidhi mahitaji ya masoko ya ndani na nje ya nchi.
Amesema mafanikio hayo yameifanya Singida kuendelea kujijengea heshima katika ramani ya dunia kama moja ya maeneo yanayozalisha bidhaa bora za nyuki, huku bidhaa za Kijiji cha Nyuki zikiendelea kuuzwa katika mataifa mbalimbali duniani.
"Kupitia ubunifu, tafiti na uwekezaji katika sekta ya ufugaji nyuki, tunaendelea kuitangaza Singida kimataifa na kufungua fursa mpya za biashara kwa wazalishaji wa mazao ya nyuki," amesema Kiemi.
Katika hatua nyingine ya kuimarisha ushirikiano wa kimataifa, Kijiji cha Nyuki kimeingia makubaliano ya kushirikiana na nchi ya Namibia, yakilenga kubadilishana ujuzi, teknolojia na uzoefu katika ufugaji wa nyuki, uchakataji wa mazao ya nyuki pamoja na maendeleo ya biashara ya bidhaa hizo.
Ushirikiano huo unatarajiwa kuongeza uwezo wa uzalishaji, kuimarisha ubora wa bidhaa na kufungua masoko mapya ya kimataifa, hatua ambayo itaendelea kuinufaisha Singida na Tanzania kwa ujumla kupitia sekta ya ufugaji nyuki.
Kwa mafanikio haya, Kijiji cha Nyuki kinaendelea kuwa mfano wa taasisi inayochangia kukuza uchumi, kuongeza thamani ya mazao ya asili na kuitangaza Tanzania katika soko la dunia kupitia bidhaa za nyuki zenye viwango vya kimataifa.
Na Abdul Ramadhani Tanzania



0 Comments