VISION CARE FOUNDATION YATOA MATIBABU NA MIWANI BURE, YAIMARISHA AFYA YA MACHO SHULENI NA JAMII

                                

Wananchi wa Mkoa wa Singida wamepata fursa ya huduma muhimu za afya ya macho kupitia kambi maalum ya upimaji wa macho, matibabu na ugawaji wa miwani bure iliyoendeshwa na Vision Care Foundation katika Shule ya Abeti, Halmashauri ya Manispaa ya Singida.

Kambi hiyo, iliyowaleta pamoja wanafunzi, walimu na wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa huo, imelenga kubaini mapema matatizo ya macho, kutoa matibabu stahiki na kuongeza uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa kulinda afya ya macho.

Akizungumza wakati wa shughuli hiyo, Mwenyekiti wa Vision Care Foundation, Eden R. Mashayo, alisema afya bora ya macho ni nguzo muhimu katika kuinua kiwango cha elimu, kuongeza tija ya uzalishaji na kuboresha maisha ya wananchi.

"Afya bora ya macho ni msingi wa elimu bora na maisha yenye tija. Kupitia ushirikiano kati ya walimu, wataalamu wa afya na jamii, tunaweza kuwafikia mapema wenye changamoto za macho na kuwapatia huduma stahiki kwa wakati," alisema Mashayo.

Alieleza kuwa mafanikio ya programu hiyo yanatokana na mkakati wa kuwajengea uwezo walimu kufanya uchunguzi wa awali wa afya ya macho kwa wanafunzi. Kupitia mafunzo hayo, walimu wameweza kutambua mapema wanafunzi wenye dalili za matatizo ya kuona na kuwaelekeza kwenye kambi kwa uchunguzi wa kina, matibabu na kupatiwa miwani pale inapohitajika.

Mashayo alisema mfumo huo wa uchunguzi wa mapema unasaidia kupunguza athari za matatizo ya macho yanayoweza kuathiri maendeleo ya kielimu kwa watoto, huku ukiongeza nafasi ya wanafunzi kushiriki kikamilifu katika masomo yao.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), zaidi ya watu bilioni 2.2 duniani wanaishi na tatizo la uoni au upofu, na takribani asilimia 50 ya matatizo hayo yanaweza kuzuilika au kutibiwa endapo yatagunduliwa mapema. Takwimu hizo zinaonesha umuhimu wa huduma za uchunguzi wa macho katika jamii, hususan kwa watoto wa umri wa kwenda shule.

Aidha, Mashayo aliwashukuru walimu kwa ushirikiano mkubwa walioutoa katika utekelezaji wa mradi huo pamoja na wananchi wa Singida kwa kujitokeza kwa wingi kutumia huduma hizo za bure, akisema mwitikio huo unaashiria kuongezeka kwa uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa afya ya macho.

Pia alitoa shukrani kwa Serikali ya Mkoa wa Singida, Wizara ya Afya pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuweka mazingira rafiki yanayowezesha wadau wa sekta ya afya kushirikiana na Serikali katika kuboresha huduma za afya kwa wananchi.

Kambi hiyo imeandaliwa chini ya School Based and Community Eye Health Project, mradi unaotekelezwa na Vision Care Foundation ukilenga kuimarisha afya ya macho kwa wanafunzi na jamii kupitia uchunguzi wa mapema, matibabu, elimu ya afya ya macho na kuimarisha mfumo wa rufaa.

Kupitia programu hiyo, Vision Care Foundation inaendelea kuchangia juhudi za Serikali katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya ya macho, hatua inayochangia kuboresha ufaulu wa wanafunzi, kuongeza tija katika jamii na kuimarisha ustawi wa wananchi wa Mkoa wa Singida.

Na Abdul Ramadhani Tanzania

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560

Post a Comment

0 Comments