
KIZIMKAZI, ZANZIBAR: Viongozi wa Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), wakiongozwa na Waziri wa Nchi, Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, wamefika nyumbani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Kizimkazi, Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar, kutoa pole na kumfariji kufuatia msiba wa kuondokewa na mume wake, Marehemu Maalim Hafidh Ameir Hassan.
Ziara hiyo imefanyika ikiwa ni sehemu ya kuungana na Rais Samia pamoja na familia katika kipindi cha maombolezo na kutoa salamu za pole kufuatia msiba huo.
Prof. Shemdoe ameambatana na Naibu Katibu Mkuu OWM–TAMISEMI, Bw. Sospeter Mtwale, pamoja na Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Miundombinu, Mhandisi Rogatus Mativila.
Viongozi hao wamewasilisha salamu za pole kutoka OWM–TAMISEMI, huku wakimtakia Rais Samia afya njema, subira, faraja na utulivu katika kipindi hiki cha maombolezo.
Aidha, wamewapa pole wafiwa wote na kuwaombea moyo wa uvumilivu na ustahimilivu katika kipindi hiki kigumu cha kumpoteza mpendwa wao.
Msiba huo umeendelea kuwakutanisha viongozi, taasisi na wananchi mbalimbali kutoa pole kwa Rais Samia na familia yake, wakionesha mshikamano na kuungana nao katika kipindi cha majonzi.


0 Comments