Hatua hizo zinaenda sambamba na wito wa wataalamu wa hali ya hewa na mamlaka mbalimbali kwa wananchi na viongozi kuchukua hatua za mapema, ikiwemo kusafisha mitaro, mifereji na maeneo yanayoweza kuzuia mtiririko wa maji.
Akizungumza kuhusu maandalizi hayo, Mkuu wa Wilaya ya Singida, Godwin Gondwe, amewapongeza wananchi wa Singida kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika kutekeleza hatua mbalimbali zinazolenga kulinda mazingira, usalama wa wananchi na mali zao.
Gondwe amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya wananchi, viongozi wa Serikali na taasisi mbalimbali katika kuhakikisha mazingira yanaendelea kuwa safi na salama, hasa katika kipindi ambacho tahadhari za msimu wa mvua zinatolewa.
Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya amewataka wananchi kuendelea kuchukua hatua za tahadhari mapema kwa kusafisha maeneo yanayozunguka makazi yao, kuondoa taka kwenye mitaro na kuhakikisha njia za maji hazizuiwi na taka au vitu vingine.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Manispaa ya Singida, Bi. Joanfaith Kataraia, ameendelea kusimamia utekelezaji wa maelekezo ya kuhakikisha usafi wa mazingira unapewa kipaumbele katika maeneo ya biashara, shule, stendi na maeneo mengine ya Manispaa.
Taarifa ya Manispaa iliyotolewa awali ilieleza kuwa usafi wa mitaro na mifereji ni muhimu katika maandalizi ya msimu wa mvua, ili kusaidia kuzuia maji kutuama na kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza.
Ushirikiano unaoendelea kati ya uongozi wa Wilaya, Manispaa na wananchi unaweka msisitizo katika uwajibikaji wa pamoja wa kulinda mazingira, huku wananchi wakihimizwa kutekeleza wajibu wao katika maeneo wanayoishi na kufanya shughuli zao.
Gondwe amesisitiza ujumbe wa mshikamano wa wananchi wa Singida kwa kauli:
“SINGIDA NAMBA MOJA, TUENDELEE KUSHIRIKIANA KULINDA MAZINGIRA NA USALAMA WA JAMII.”
Kwa hatua hizi, Singida inaendelea kujenga utamaduni wa maandalizi ya mapema, usafi wa mazingira na ushirikiano kati ya Serikali na wananchi katika kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa.
Na Abdul Ramadhani
BANDOLA MEDIA

0 Comments