Taasisi ya LBL Loyality Team imetoa Msaada wa vitu mbalimbali katika Shule ya Msingi Kizega wilayani Iramba mkoani Singida ili kupunguza baadhi ya changamoto zinazowakabili wanafunzi shuleni hapo.
Akizungumza baada ya kutoa msaada huo Kiongozi wa LBL Loyality Team RODA BENZI alisema wametoa msaada huo baada ya kuguswa na changamoto zinazokabili wanafunzi hao, na kuona ni vyema wakatoa japo kidogo ili kiweze kuwasaidia wanafunzi.
BENZI alisema kukosekana kwa baadhi ya mahitaji kwa wanafunzi husababisha wanafunzi kushindwa kufanya vizuri katika masomo yao, hivyo LBL iliona umuhimu wa kutoa msaada ili waweze kupunguza changamoto ili wanafunzi wafanye vizuri katika masomo yao.
Hata hivyo BENZI alitoa wito kwa Jamii kuona kuwa kunasababu ya kuwasadia wanafunzi wote wenye mahitaji maalum ili kuisaidia serikali kutatua changamoto za wanafunzi na waweze kutimiza ndoto zao za kupata Haki yao ya Msingi ya kupata Elimu.
Alisema LBL Royality Team itaendelea kutoa ushirikiano kwa Serikali katika kutoa misaada kama hiyo ili iweze kuondoa au kupunguza changamoto mbalimbali za wanafunzi na watu wengine wenye Mahitaji maalum katika Jamii.
Kwa upande wake Mwl. Mkuu Msaidizi Shule ya Msingi Kizega CHRISTOPHER KIRUMBI alisema licha ya Serikali kuendelea kutoa Mahitaji kwa Wanafunzi wenye mahitaji maalum wa Shule hiyo, bado wanafunzi hao wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo Mavazi, Sare za Shule, Mafuta kwa Watoto wenye Ualibino na Maandishi ya Nukta Nundu kwa wanafunzi wasioona.
KIRUMBI alisema changamoto hizo zinazokwamisha juhudi za wanafunzi hao katika masomo yao, hivyo ameiomba Jamii na Taasisi mbalimbali kuwasaida wanafunzi hao ili waweze kutimiza ndoto zao za kupata Elimu.
Nao baadhi ya wanafunzi wameishukuru Taasisi ya LBL Loyality Team kwa msaada huo ambao utawasaidia kupunguza changamoto zinazowakabili shuleni hapo.
Wanafunzi hao wameziomba Taasisi na Mashirika mbalimbali kutoa msaada kwa wanafunzi ambao wana mahitaji maalum ili waweze kutimiza ndoto zao za kupata Elimu kama ilivyo kwa wanafunzi wengine.
Shule ya Msingi Kizega ina wanafunzi Jumuishi ambao hawana ulemavu na wenye mahitaji maalumu ikijuimuisha wanafunzi wenye Ulemavu wa Ngozi (Albino), Ulemavu wa Viungo, Uoni hafifu na Vipofu.
0 Comments