Recent-Post

KENEDY JUMA:ILIKUWA NDOTO YANGU KUCHEZA MASHINDANO YA KIMATAIFA

KENEDY Juma, beki wa Simba amesema kuwa kwa muda ambao amepewa kwenye muda wa mechi za kimataifa licha ya kutomaliza dakika 90 kwake ni somo na ndoto ambayo imetimia.

Kenedy ambaye ni ingizo jipya ndani ya Simba aliibuka huko akitokea Klabu ya Singida United ni mara yake ya kwanza kushiriki mashindano ya kimataifa na timu yake imetinga hatua ya makundi.

Mechi yake ya kwanza kimataifa ilikuwa dhidi ya AS Vita ya Congo na aliyeyusha dakika tatu uwanjani kwa kuwa alinyanyuliwa kutoka benchi.

Mchezo huo chini ya Didier Gomes ambaye ni Kocha Mkuu wa Simba, baada ya dakika tisini ubao ulisoma AS Vita 0-1 Simba huku bao la ushindi likifungwa na Chris Mugalu kwa mkwaju wa penalti.

Pia alikuwa sehemu ya kikosi kilichomaliza kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Al Ahly ambapo alitumia dakika 4 kwa kuwa alianza benchi kwenye mchezo huo ambao ni gumzo ndani ya bara la Afrika.

Beki huyo amesema:"Nilijua kwamba siku moja ningecheza mashindano ya kimataifa baada ya kuwa ndani ya Simba hiyo ni ndoto yangu na imetimia kwa kweli ninafurahi kuona inakuwa hivyo.

"Licha ya kwamba ni muda mfupi ambao ninautumia ndani ya uwanja kwenye mechi za kimataifa hiyo kwangu ni nzuri kwani ninajenga uzoefu na ninazidi kuwa bora," amesema.

Leo kikosi cha Simba kinatarajiwa kukwea pipa kuelekea nchini Sudan kwa ajili ya mchezo wao wa kundi A dhidi ya Al Merrikh mchezo huo unatarajiwa kuchezwa Machi 6.

 

Post a Comment

0 Comments