Kamati za kudumu za Bunge zinatarajia kuanza kukutana siku ya Jumatatu wiki ijayo tarehe 8 hadi 26, Machi, 2021 ambapo Wabunge wote wanatakiwa kuwasili jijini Dodoma Jumapili Tarehe 7 ,Machi, kwa ajili ya vikao hivyo.
Katika taarifa iliyotolewa kwa Vyombo vya Habari leo na kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa kimataifa, Ofisi ya Bunge imefafanua kuwa shughuli za kamati zitakakuwa katika kipindi hicho ni pamoja na kupokea mapendekezo ya serikali kuhusu mpango, kiwango cha ukomo wa Bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2021/2022 kwa mujibu wa kanuni ya 116[1] ya kanuni za kudumu za Bunge toleo la Juni, 2020, wabunge wote watahusika.
Shughuli zingine zitakazofanyika ni pamoja na kutembelea na kukagua utekelezaji wa miradi iliyotengewa fedha kwa mwaka wa fedha 2020/2021 ili kuzingatia masharti ya kanuni ya 117[1] ya kanuni za kudumu za Bunge toleo la Juni 2020 ambapo wajumbe wa kamati za kisekta watahusika.
Taarifa ya kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa kimataifa ,Ofisi ya Bunge iliendelea kubainisha kuwa shughuli zingine zitakazofanyika ni uchambuzi wa sheria ndogo zilizowasilishwa katika mkutano wa pili wa Bunge ili kutekeleza masharti ya kifungu cha 11 cha nyongeza ya Nane ya kanuni za kudumu za bunge toleo la Juni,2020 na mashauriano kati ya kamati ya Bajeti kuhusu masuala muhimu yatakayokuwa yamejitokeza kwenye kamati za kisekta wakati wa uchambuzi wa taarifa za utekelezaji wa Bajeti kwa mwaka wa fedha 2019/2020.
0 Comments