Mirerani. Changamoto ya walimu wa shule ya msingi Songambele wilayani Simanjiro Mkoa wa Manyara kujisaidia choo kimoja na wanafunzi imepatiwa ufumbuzi baada ya diwani wa Mirerani, Salome Mnyawi kuwajengea choo.
Mnyawi wakati akikabidhi choo hicho leo Alhamisi Machi 4, 2021 amesema pia amenunua magunia ya mahindi na maharage ili wanafunzi hao wale chakula shuleni.
"Nimetimiza ahadi yangu ya kuwajengea walimu choo kwa gharama zangu, nikawanunulia chakula magunia mawili ya mahindi na moja la maharage kisha mdau wangu Rachel Njau akawanunulia wanafunzi yatima 24 sare za shule," amesema Mnyawi.
Njau ambaye ni katibu wa chama cha wachimbaji madini mkoani Manyara (Marema) tawi la Mirerani amesema baada ya Mnyawi kumweleza changamoto ya sare za wanafunzi hao alinunua mashati, sketi, kaptula, nguo za ndani na soksi.
0 Comments