Rais Samia Suluhu Hassan Septemba 14 atazindua kitabu cha mkakati wa uelimishaji na uhamasishaji wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 jijini Dodoma.
Taarifa hiyo imetolewa leo Septemba 12, 2021 na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusu shughuli hiyo aliyosema inalenga kuandaa umma na wadau kuhusu sensa ya watu na makazi mwakani.
Mkuu wa Mkoa amesema uzinduzi huo unaokwenda na kauli mbiu ya ‘Sensa kwa maendeleo, jiandae kuhesabiwa’ utafanyika Septemba 14 uwanja wa Jamhuri jijini hapa kuanzia saa 1 asubuhi
Kwa mujibu wa Mtaka, viongozi mbalimbali watahudhuria akiwemo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa atakayekuwa mwenyeji na Mwenyekiti mwenza kutoka Zanzibar ambaye ni Makamu wa pili wa Rais Hemed Suleiman Abdallah.
Viongozi wengine ni Kamisaa wa sensa Tanzania Bara, Anne Makinda, Kamisaa wa sensa Zanzibar, Balozi Mohamed Haji Hamza, pamoja na Mawaziri, Manaibu Waziri, Makatibu wakuu, Manaibu katibu wakuu na viongozi wa serikali kutoka Mikoa minne.
Mkuu wa Mkoa amesema Viongozi wa serikali kutoka Mikoa minne ya Singida, Iringa, Morogoro na Manyara watashiriki hivyo akaomba wananchi wa wa Dodoma kujitokeza kwa wingi siku hiyo.
Kaimu Mkurugenzi wa Takwimu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Daniel Masolwa amesema Ofisi ya Taifa ya Takwimu imeshaandaa sensa ya majaribio ambayo inahusisha mikoa 13 nchini na kwamba zoezi linakwenda kwa mafanikio makubwa.
Masolwa ametaja lengo la majaribio hayo ni kupima na kuhakiki vitendea kazi kama vitakuwa na changamoto virekebishwe kabla ya kazi yenyewe ambayo alisema inafanywa na umakini na watu wenye mafunzo na weledi.
Dodoma.
0 Comments