VIONGOZI, WACHEZAJI WAMLILIA ZACHARIA HANSPOPE

 

USIKU wa Septemba 10, 2021 Klabu ya Soka ya Simba ilithibitisha kufariki dunia kwa Aliyekuwa Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Klabu hiyo, Zacharia HasPope baada ya kuugua kwa muda na kuendelea na matibabu akiwa nchini Tanzania.

Taarifa hiyo imeshtua watu wengi katika tasnia ya Soka na tasnia mbalimbali kutokana na umaarufu wa HansPope katika nafasi yake kwenye Klabu ya Simba SC, pia alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Klabu hiyo kongwe nchini.

Moja ya mtu aliyethibisha kuzungumza na HansPope akiwa amelazwa Hospitali moja hapa nchini kutokana na kuugua, ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa ambaye ameeleza kuwa Tanzania imepoteza mtu muhimu ambaye alitamani kuona Tanzania inakaa kwenye Viwango vya Kimataifa vya Soka.

Msigwa ameeleza kuwa mara ya mwisho kuwasiliana na marehemu HansPope alimjibu huku akiwa kwenye Mashine ya Oksijeni (mashine ya kumsaidia kupumua). HansPope alimueleza Msigwa kuwa, “ugonjwa unatesa sana huu” na baadaye akasisitiza watu kuchukua tahadhari.

“Poleni sana wanafamilia, uongozi wa Simba SC, wachezaji, wapenzi na wanachama, wapenzi wa soka na wote walioguswa na msiba huu”, ameandika Msigwa kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii.

Mwekezaji na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Simba SC, Mohammed Dewji ameeleza hisia zake baada ya kifo hicho cha HansPope huku akimtaja ni mmoja wa watu walioipigania Simba na kuweka maslahi mbele wakati wote bila kujali maslahi yake binafsi.

Aliyekuwa Msemaji wa Simba SC, Haji Manara amesema, “Nimechelewa sana kusikia taarifa za huu msiba wa mzee wetu Zacharia, Imenifadhaisha sana na imeniondolea Mood yangu. Kwangu alikuwa Mwanamichezo halisi shupavu na ameacha pengo kubwa Kwa mpira wetu na klabu yake Kwa ujumla, Pumzika Kwa amani Captain”.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Klabu ya Simba SC, Barbara Gonzalez amemtakia mapumziko mema marehemu HansPope huku akituma Picha wakiwa pamoja enzi za uhai wake katika majukumu yao ya kazi katika Klabu ya Simba SC.

Mchezaji wa zamani wa Simba SC, Emmanuel Okwi baada ya kusiki Kifo hicho ameandika, “Kwa mashabiki wote wa Simba SC, tumepoteza Kiongozi mwenye maono ya mbali,  Baba na Kiongozi mkubwa. Nashindwa kueleza jinsi gani inavyoumiza kumpoteza HansPope!! Tuko Pamoja Wana Simba Wote!! May His Soul Rest In Peace!!”.

Timu mbalimbali za soka nchini wakiwemo Yanga SC, Azam FC na Wachezaji wengi wa soka wameendelea kutoa salamu za rambirambi kufuatia kifo hicho cha Zacharia HansPope.

Pichani Kulia ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Simba SC, Barbara Gonzalez akiwa na marehemu Zacharia HansPope (kushoto) enzi za uhai wake, wakiwa kwenye moja ya majukumu ya Klabu hiyo ya Simba SC.
                                               Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments