Baada ya kikao Ajibu na Mkude wasema ya moyoni

KOCHA Msaidizi wa Simba, Hitimana Thiery amesema kwamba amebaini ishu ya Jonas Mkude na Ibrahim Ajibu ilikuwa ni ndogo sana.

Hitimana ameweka wazi kwamba kiwango walichoonyesha kwenye mechi ya juzi dhidi ya Namungo ilikuwa ni majibu yao kwamba sasa kila kitu kiko sawa na ni mwendo wa kazi-kazi tu.

Kocha huyo licha ya kutoweka wazi kwamba wamezungumza nini au alibaini nini, alisema kwamba alikaa nao kila mmoja kwa muda wake kama kaka yao na wakamuelewa na kuahidi mabadiliko na ubora mkubwa kwa kuanzia na mechi iliyopita na ndio maana akawaanzisha kwenye ushindi wa bao 1-0 na wakaupiga mwingi.

Hitimana alisema, Ajib ni moja ya mbadala wa Clatous Chama na Mkude naye ni kiungo fundi na wawili hao wana uwezo mkubwa.

“Nilichukua nafasi ya kukaa nao na kuwaeleza mengi kama wadogo zangu kwa kuwa natambua uwezo wao, naamini walinielewa na kuyafanyia kazi yale ambayo niliwaambia wayafanye.

“Niliwashauri wote wawili wajitahidi kuongeza sana nguvu katika mazoezi yao ili waweze kumfanya mwalimu kuwapa nafasi kwa kuwa uwezo wanao mkubwa na ndio maana wamesajiliwa Simba,” alisema.

“Nimeshukuru sana Mungu na wao nawapongeza sana kwani nimewapa nafasi wamezitendea haki, nawasihi tu waendelee na uwezo huo huo ili hata kocha ajaye aweze kuwaamini na kuwapa nafasi,” alisema Hitimana.

Mwanaspoti lilimtafuta Mkude akakiri kuzungumza na Hitimana huku akiamini namna ambavyo aliwathamini na kukaa nao kuwashauri akisema kwao ni faraja kubwa na wanajivunia hilo hivyo hawatamwangusha.

“Ni kweli kabisa, tulikaa naye kocha kama kaka yetu, alitueleza mengi na sisi tulimuelewa sana, tumeyafanyia kazi aliyotutaka tuyatekeleze na hatutomwangusha kamwe, jana tumemuonyesha kuwa hakufanya kosa kutupa nafasi,” alisema Mkude.

Mchezaji wa zamani wa Yanga, Akida Makunda alisema, wachezaji hao ni wazuri katika viwango lakini utovu wa nidhamu ndio unawagharimu.


ZAHERA NA AJIBU

Mkurugenzi wa Ufundi wa Yanga, Mwinyi Zahera amekuwa akishangazwa na jinsi benchi la ufundi la Simba linavyoshindwa kumtumia Ajibu.

Ajibu kabla ya kurudi tena Simba alikuwa chini ya Zahera kwenye kikosi cha kwanza cha Yanga na kuisaidia timu hiyo kumaliza nafasi ya pili akiwa kinara wa asisti kwenye Ligi Kuu na alipewa majukumu ya unahodha ndani ya Yanga.

“Ajibu ni mchezaji mzuri sana ana akili ya mpira tofauti na nyota wengi wa Kitanzania, shida yake ni uvivu, lakini kama kocha umeona kitu kwake huwezi kukubali kumuacha aendeleze changamoto aliyonayo,” alisema Zahera na kuongeza kuwa,

“Ni sawa na ukiwa na watoto watatu nyumbani kwako mmoja akawa mvivu unaweza kumsusa? Ni kitu ambacho hakiwezekani kwa upande wangu, niliwezana na mchezaji huyo kwasababu muda mwingi nilikuwa nakaa naye na kumuambia kuwa yeye ni bora,” alisema na kuongeza kuwa;

“Nakumbuka siku ya kwanza nimemuita nikamwambia Ajibu wewe ni mchezaji mzuri sana na ni wewe tu hakuna mwingine unatakiwa kujituma na kupambana ili kuonyesha kile ulichonacho, alinielewa na kufanya mazoezi kwa nguvu na kunisaidia kwenye kikosi changu,” alisema.

Zahera aliongeza kuwa baada ya kuona amemuelewa aliamua kumpa majukumu ya unahodha na hilo liliongeza upambanaji wa mchezaji huyo hivyo amewataka makocha wanaomfundisha mchezaji huyo kutomsusa na badala yake wamjenge kisaikolojia.

“Ukikaa na Ajibu na kumwambia nini anatakiwa kufanya ni muelewa, hawezi kuacha kufanya lakini ukimtenga kama hivi wanavyofanya makocha waliopita hapo ni kumkosea na kuharibu kipaji alichonacho,” alisema Zahera.


SIMBA SIKU NNE

Simba imewapa mapumziko ya siku nne wachezaji wake ambapo watatakiwa kurejea katika majukumu yao ya kawaida Jumatatu kuendelea na maandalizi ya mwendelezo wa ligi baada ya kusimama kupisha majukumu ya timu za Taifa.

“Wiki ijayo tutarejea na kuendelea na majukumu yetu kama kawaida, kwa wachezaji wale ambao hawatakuwa na majukumu ya timu zao za Taifa,” alisema Hitimana.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments