Namtumbo yaongoza kwa utoaji chanjo ya UVIKO-19 mkoani Ruvuma

 NA YEREMIAS NGERANGERA


HALMASHAURI ya Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma imeongoza katika zoezi la utoaji chanjo ya virusi vya Korona (UVIKO-19).

Akisoma taarifa ya chanjo kwa mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge, Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo, Dkt. Julius Kenneth Ningu amesema wilaya ya Namtumbo inaongoza katika mkoa wa Ruvuma katika kuchanja wananchi wake chanjo ya Uviko 19 aina ya Sinopharm.

Dkt.Ningu amesema hayo katika ziara ya Mkuu wa mkoa waRuvuma wilayani Namtumbo katika Kata ya Luchili kuzungumza na wananchi wa kata hiyo ili kutatua mgogoro wa makao makuu ya kata ambao wananchi wa kata hiyo wanagombania.

Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo Lucia Kafumu amesema, sababu kubwa ya kuchanja wananchi wengi wilaya ya Namtumbo ilikuwa ni uelewa walioupata kuhusu elimu kutoka kwa watalaamu wa afya, viongozi wa serikali, dini ,chama na kwa kushirikiana na wananchi wengine katika vijiji mbalimbali wilayani humo walioweza kusaidia kutoa elimu kwa wananchi wenzao.

Kafumu amedai wakati timu ya wataalamu wa afya inapita kutoa elimu katika vijiji kwa njia ya mikutano ya hadhara ilipata ushirikiano wa viongozi wa serikali,viongozi wa dini,chama na baadhi ya wananchi ambao walijitokeza kuelimisha wananchi wenzao.

Aidha, Kafumu amesema kitendo cha viongozi wa serikali kutoka katika vijiji vya wilaya ya Namtumbo kujitokeza kuchanja ndicho kilichosaidia hata wananchi wengi wajitokeze katika kupata chanjo baada ya kuona viongozi wao kuchanja na hata sasa wananchi wanajitokeza kwa wingi katika zahanati zao kuchanja.

Mratibu wa chanjo katika Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo, Elias Patrick Boniface alisema wilaya ya Namtumbo ilipokea chanjo dozi 5300 ya UVIKO 19 aina ya Sinopharm tarehe 27mwezi Oktoba, mwaka huu na kuzisambaza katika vituo vya kutolea huduma za afya na kufikiatarehe 31 mwezi Oktoba, mwaka huu dozi hizo ziliisha na kufikia asilimia 100 katika Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo.

Tathimini ya uchanjaji mkoa wa Ruvuma inaonyesha kuwa, Wilaya ya Namtumbo ni ya kwanza kwa kuchanja ikifuatiwa na Halmashauri ya Mbinga na ya tatu ni halmashauri ya Tunduru huku Halmashauri ya Nyasa ikiwa nafasi ya nne

Zingine ni Halmashauri y Songea Manispaa ambayo imeshika nafasi ya 5,na Halmashauri ya Madaba imeshika nafasi ya sita huku Halmashauri ya Mbinga Mji ikishika nafasi ya saba na Halmashauri ya Songea ikishika nafasi 8 kimkoa katika uchanjaji.

Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo ina jumla ya vituo vya kutolea huduma za afya 54 zinazohusika na utoaji wa huduma za chanjo ya Uviko-19 ya Sinopharm ambavyo wananchi wanavitumia katika kupata chanjo hiyo na kusababisha wilaya kuongoza katika mkoa katika zoezi la uchanjaji.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments