Mvua ya upepo yaezua mapaa Handeni

Mvua ya upepo iliyonyesha juzi katika Kata ya Ndolwa, Halmashauri ya Wilaya Handeni, mkoani Tanga imezua paa za vyumba vya madarasa manne na ofisi ya Shule ya Msingi Luye iliyopo Kata hiyo.

Akizungumza leo Ijumaa Januari 21, 2022 Mkuu wa Wilaya ua Handeni, Siriel Mchembe amewahakikishia wazazi na wanafunzi ndani ya wiki mbili ukarabati utakuwa umekamilika.

Mchembe amesema vyumba vine vya madarasa pamoja na ofisi ya walimu vimeezuliwa na paa hivyo amewataka wananchi kushirikiana na Serikali kuhakikisha ukarabati unafanyika haraka.

"Timu ya mkurugenzi imeshapita na kufanya tathimini  ya vitu ambavyo vinahitajika,hivyo mkurugenzi amenihakikishia ndani ya siku 14 wanafunzi watarudi darasani na wengine wataendelea na masomo kwenye shule shikizi ya jirani",amesema Mchembe.

Akielezea hali hiyo mwalimu mkuu wa shule ya msingi Luye, Hossein Mwesange amesema saa nane mchana ilitokea mvua kubwa iliyoambatana na upepo na kuezua madarasa hayo ila hakuna mwanafunzi wala mwalimu aliyeathirika

Amesema wanafunzi 300 watakosa masomo kwa zaidi ya wiki moja kutokana na madhara hayo, kwani hakuna madarasa ya ziada ambayo wataweza kusoma.

 

Post a Comment

0 Comments