RC SINGIDA ATEMBELEA MGODI WA SHANTA GOLD ATAKA USHIRIKIANO

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge (mwenye koti la bluu) akiangalia moja ya eneo la machimbo ya dhahabu Mara baada ya kutembelea Kampuni ya Shanta Gold inayoendesha shughuli hizo  katika kijiji Cha Mang'onyi Wilaya ya Ikungi.

RC.Mahenge  akiendelea na ukaguzi wa Mgodi wa machimbo ya dhahabu unaomilikiwa na Kampuni ya Shanta Gold.

Ukaguzi wa mgodi huo ukiendeleaZiara unaendelea
Ukaguzi ukiendelea.
 WAWEKEZAJI  mkoani Singida wametakiwa kushirikiana na Halmashauri za wilaya wakati wa kuanzisha 

miradi ya Maendeleo ya Kijamii  (Community socially responsibility – CSR ) ili kukubaliana aina za miradi na namna itakavyotekelezwa lengo likiwa ni  kuepuka matumizi makubwa ya fedha kwa kazi ambazo zingetumia fedha kidogo.

Ushauri huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa huo Dk. Binilith Mahenge leo January 26, 2022 alipotembelea machimbo ya madini ya dhahabu yanayochimbwa na Kampuni ya  Shanta Gold iliyopo Kijiji cha Mang’onyi wilayani Ikungi ambapo alieleza kwamba miradi yote inayoanzishwa na wawekezaji ipitie katika Halmashauri za wilaya ambazo zinafahamu mahitaji ya wahusika na  gharama halisi za ujenzi katika maeneo hayo.

Akitolea mfano kwa madarasa yaliyokamilika hivi karibuni kupitia fedha za uviko 19  Mahenge alisema kila darasa liligharimu kiasi cha Sh.milioni 20, ikilinganishwa na madarasa yaliyojengwa na Shanta Gold ambayo yamegharimu Sh.milioni 28 kwa kila darasa.

“Kama mradi huu mgeshirikisha Halmashauri kwa kiasi kikubwa mngetumia Force Account na mngepata wakandarasi wa bei ndogo na fedha zingebaki zikafanya maendeleo mengine katika jamii. Niwashauri mshirikiane ipasavyo na Halmashauri kupanga aina ya miradi mnayotaka kuipeleka kwa jamii”, alisema Mahenge.

Hata hivyo Mahenge ameipongeza kampuni hiyo ya Shanta Gold  kwa kutumia zaidi ya milioni 190 kwa kupeleka huduma kwa jamii ikiwemo ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa na uchimbaji wa visima vya maji huduma ambazo zinafaidisha vijiji vya Mang’onyi, Sambaru, Mlumbi, Tupendane na Mwau.

Aidha, Dkt. Mahenge ameitaka jamii inayozunguka mgodi huo kutumia fursa na kuwa wabunifu kwa kuanzisha miradi mbalimbali ikiwemo ufugaji wa kuku na mama lishe pamoja na kuomba ajira katika kampuni hiyo kwa kuwa kadri mradi unavyokuwa ndivyo mahitaji yatakavyoongezeka.

Awali akitoa taairifa ya mgodi Meneja wa mradi huo Kundael Mtiro alisema mpaka kufikia sasa mradi ulitakiwa kufikia asilimia 46.14 katika utekelezaji wake lakini kwa sababu ambazo zimekuwa nje ya uwezo mpaka sasa utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 43.62 .

Hata hivyo Mtiro  akaendelea kufafanua kwamba mpaka Juni,2022 mradi utakuwa unakamilisha  robo ya nne ya mwaka ambapo wanategemea kwamba utakuwa umekamilika kwa kuwa tayari washasimika mabomba katika maeno yote yanayohusika pamoja na uchimbaji wa visima, ujenzi wa ofisi na makazi umekamilika kwa asiliami 80.

Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Jerry Murro alisema mgodi huo utainua uchumi wa Singida na taifa kwa ujumla ambapo utasisimua sekta nyingine za elimu barabara, zahanati na wananchi kupata ajira.

Alisema wilaya imeendelea kusimamia hali ya usalama katika eneo la mradi na imehakikisha wanachi wote waliokuwa wanastahili kupata fidia zao wamelipwa kwa wakati.

Na Mwandishi Wetu, Singida

 

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments