Chanjo ya Ukimwi kuleta matumaini mapya kufanikiwa

Imeelezwa kuwa, kuna changamoto nyingi katika utafiti wa chanjo ya Virusi vya Ukimwi (VVU)lakini haimaanishi kushindwa. Dk Marianne Mureithi wa Taasisi ya Mpango wa Chanjo ya Ukimwi Kenya kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi (KAVI-UoN) alisema hayo katika mahojiano yake na Mtandao wa Healthy Nation wa Kenya.

Alisema tafiti zimekuwa zikifanyika kupata chanjo ya VVU lakini bado kuna changamoto kadhaa za kitaalamu.

“Majaribio ya chanjo ya VVU hayajashindwa, badala yake tumejifunza mengi kutokana na majaribio ya awali, ambayo yanatoa matumaini kuelekea mafanikio yake,” alisema Dk Mureithi.

“Ulimwengu ulio na chanjo ya VVU utakuwa na afya zaidi kuishi,” alisema Profesa Omu Anzala ambaye ni mtaalamu wa virusi na mtafiti mkuu wa kimatibabu anayefanya kazi katika Taasisi ya Kavi.

Jitihada za kupata chanjo ya VVU zilianza miongo minne iliyopita, wakati maambukizi ya VVU kwa binadamu yalipogunduliwa miongo kadhaa iliyopita.

Alisema awali, kulikuwa na matumaini ya haraka kupata chanjo kutoka kwa jumuiya ya wanasayansi.

Majaribio ya kutafuta chanjo

Utafutaji wa chanjo ulianza na uongozi wa Margaret Heckler, ambaye wakati huo alikuwa Waziri wa Afya wa Marekani na Huduma za Kibinadamu wa Marekani.

Heckler alikuwa na matumaini kwamba chanjo ya VVU ingekuwa tayari kwa miaka miwili, lakini msaidizi wake Edward Brandt, alitilia shaka kuwa chanjo hiyo ingepatikana ndani ya muda mfupi.

“Hakuna anayejua kwa hakika itachukua muda gani kutengeneza chanjo hiyo, ingawa uvumi wa jumla ni kwamba itapatikana kutokana na uchunguzi wa kimatibabu ndani ya miaka miwili au mitatu,” alinukuliwa na mtaalamu wa VVU wa Marekani Jose Esparza katika Jarida la kisayansi la ‘Elsevier’.

Baadaye ilidhihirika kuwa Brandt alikuwa sahihi kwa sababu miaka 40 baadaye, majaribio mengi ya kupata chanjo ya VVU yalifanywa lakini hakuna lililofaulu.

“Wakati huo hakuna aliyejua kwamba ugonjwa wa Ukimwi ulikuwa mgumu zaidi kupata chanjo yake ikilinganishwa na magonjwa mengine ya virusi ambayo chanjon zake zilipatikana kwa mafanikio,” alisema Esparza.

Hata hivyo, wazo la Heckler lilihuishwa na wanasayansi wa Ufaransa wakiongozwa na Daniel Zagury, aliyekuja Afrika mwaka 1987 kufanya majaribio ya kwanza ya chanjo ya VVU.

Majaribio hayo yaliendeshwa katika nchi ambayo baadhi ya wanasayansi wanaamini kuwa ndiyo chimbuko la VVU, yaani Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Thailand, mwaka wa 1990, ikawa nchi ya kwanza iliyoendelea kuwa na majaribio ya chanjo ya VVU kwa binadamu, ambayo yalihusisha takriban watu 2,500.

Kenya, jaribio la kwanza la kimatibabu lilifanyika mwaka wa 2001 na liliongozwa na muungano wa kimataifa ikiwa ni pamoja na Mpango wa Kimataifa wa Chanjo ya Ukimwi (IAVI), Chuo Kikuu cha Oxford, na Kavi-Institute of Clinical Research katika Chuo Kikuu cha Nairobi.

Hadi sasa, Kavi-UoN imefanya majaribio ya kimatibabu ya chanjo ya VVU zaidi ya 18, iko kwenye majaribio ya awamu ya tatu ya chanjo ya VVU katika jitihada ya kupata chanjo yenye ufanisi.

Wanasayansi wa Kavi walisema chanjo yenye kuchukua muda mrefu ndiyo itakuwa na ufanisi wa kukomesha VVU.

Hata hivyo, walikubali kuwa utafiti huo utachukua muda mrefu kupata chanjo yoyote ile.

Majaribio ya awamu ya kwanza na pili hutoa data kuhusu usalama wa chanjo na uwezo wao wa kuathiri majibu ya kinga mahususi kwa VVU.

Wiki moja iliyopita, wataalamu kutoka Kavi ilitangaza kuwa, watakuwa wakifanya majaribio ya kliniki ya chanjo ya VVU kwa binadamu kwa kutumia teknolojia ya mRNA.

Utafiti huo unafanywa Marekani na watu 56 wasio na VVU watapatiwa chanjo hiyo ambayo ni ya kwanza na ya aina yake.

Dk Mureithi aliwatoa hofu baadhi ya watu, kwamba mRNA haiingiliani na muundo wa chembe za urithi bali inahusika na protini katika mwili na kuboresha mfumo wa kinga.

“Chanjo zinazofanana za DNA ambazo pia haziingiliani na muundo wa jeni zimejaribiwa kwa miaka mingi na kuthibitishwa kuwa salama,” alisema Dk Mureithi.


Ugumu wa utafiti wa chanjo ya VVU

Tatizo moja la VVU liko ndani sana, kwa maana ya kwamba kila mtu anayeishi na VVU ana virusi tofauti na mwingine. Na katika kiwango cha kimataifa, utofauti wa virusi ni mkubwa sana.

Chanjo za awali hazijatoa kingamwili zinazoweza kuzuia aina zote zilizopo za VVU.

“Hata hivyo, tumegundua kuwa baadhi ya watu wanaoishi na VVU kwa kawaida hutengeneza kinga mwili maalumu ambazo huzuia karibu aina zote za VVU na kingamwili hizo huitwa bNABs,” alisema Profesa Anzala.

Baadhi ya kingamwili hizo zimetambuliwa awali katika taasisi ya Kavi kwa ushirikiano na IAVI. Dk Daniel Muema ambaye ni mwanasayansi wa utafiti , alisema matangazo ya hivi majuzi yanadokeza ukweli kwamba ulimwengu unakaribia kupata chanjo ya VVU yenye ufanisi.

“Teknolojia ya mRNA, lengo kuu la chanjo zinazozalishwa kwa kutumia jukwaa hili ni kwamba zinashawishi kingamwili (bnAbs), ambazo zimeonyesha kuzuia maambukizi ya VVU.

“Ingawa chanjo nyingi kama zile za Uviko-19 zinaundwa ili kupunguza ukali wa ugonjwa, lengo la chanjo ya VVU ni kuzuia maambukizi kwanza,” alisema Dk Mureithi.

Dk Robert Lang’at ambaye ni mwanasayansi mtafiti kutoka Kavi, alisema chanjo yenye mafanikio dhidi ya VVU bila shaka itabadilisha udhibiti wa VVU.

Mwaka jana, utafiti wa chanjo ya VVU uitwao ‘Imbokodo’ haukufanikiwa kwa kuwa, watafiti waligundua kuwa inaweza tu kuzuia maambukizi ya VVU kwa asilimia 25.2, chini ya kiwango kinachohitajika cha asilimia 50, au zaidi.

Jaribio lingine kubwa la kliniki la chanjo ya VVU Afrika Kusini lililopewa jina la ‘Uhambo’ pia lilisitishwa kwa sababu ya ufanisi mdogo na kati ya zaidi ya washiriki 120 ambao walikuwa wamechanjwa walikuwa wameambukizwa VVU.


Hatua nyingine

Katika azimio la Paris, Ufaransa lililoitwa ‘Paris Declaration Commitments’ lililotiwa saini mwaka wa 2014, mojawapo ya ahadi ambazo zimetekelezwa na Kenya ni kwamba nchi zinapaswa kufikia lengo la 90:90:90 ifikapo mwaka 2020.

Hii ina maana asilimia 90 ya watu wanaoishi na VVU wanajua hali zao, asilimia 90 ya walioambukizwa wanatumia dawa za kufubaza VVU; na asilimia 90 ya wale wanaopata matibabu wamepunguza kiwango cha virusi vyao kwa kiwango kikubwa.

Nchi nyingi bado hazijafikia lengo hilo. Hata hivyo, miongo kadhaa ya utafiti wa chanjo ya VVU imewafundisha wanasayansi mengi kuhusu mfumo wa kinga.

Kwa mujibu wa kikundi Kazi cha Ufuatiliaji wa Rasilimali kwa Utafiti na Maendeleo ya Kuzuia VVU, mradi wa Shirika la Utetezi la AVAC, takriban Sh1.6 trilioni za Kenya zilitumika katika utafiti wa chanjo ya VVU kati ya 2000 na 2018.

Takwimu zinaonyesha kuwa hadi sasa, kumekuwa na majaribio makubwa matano ya ufanisi wa chanjo ya Awamu ya 3 dhidi ya VVU, kila moja kwa gharama ya zaidi ya dola milioni 100 za Marekani.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments