Simu Janja, Lifti Za Bodaboda Kichocheo cha VVU Kwa Wasichana


Tamaa. Ndivyo inavyotafsirika baada ya kuzungumza na msichana mwenye umri wa miaka 16 aliyepata maambukizi ya virusi vya Ukimwi (VVU).

Anasema licha ya kupata mahitaji yote kwa wazazi wake, aliathiriwa na makundi rika yaliyomfanya ahusudu mambo mengine kuliko kile kilichompeleka shuleni.

Nikiwa kidato cha pili nilipata marafiki ambao walikuwa ni wajanja na wanaokwenda na wakati pale shuleni. Wikiendi walinishauri twende beach na huko walinifundisha baadhi ya tabia ikiwemo kuvuta shisha.

“Walikuwa na marafiki wa kiume na siku moja baada ya kufanya starehe nilipitiwa na usingizi na niliposhtuka nilijikuta nipo na mtu nisiyemfahamu. Niliogopa na niliporudi nyumbani ikawa siri yangu,” anaeleza binti huyo anayesoma kidato cha tatu katika shule mojawapo iliyopo jijini Dar es Salaam.

Anasema aligundulika kuwa na maambukizi ya VVU baada ya kupima kwa hiyari yake kutokana na elimu aliyoipata kuhusu maambukizi ya ugonjwa huo.

Hata hivyo, anasema hakuwahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi, lakini tendo la siku moja lilimpa maambukizi ya VVU.

“Ilikuwa vigumu sana kupokea matokeo, kujikubali na kuwashirikisha wazazi,” anasema binti huyo ambaye ameshaingia katika mpango wa kutumia dawa za kufubaza virusi hivyo (ARV).

Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, wasichana wawili mpaka watatu wenye umri kuanzia miaka 15 hadi 24 huambukizwa VVU kila baada ya saa moja nchini.

Akizungumzia hilo, Mkurugenzi mtendaji wa Shirika Dare, Dk Lilian Mwakyosi anasema simu janja ni moja ya sababu kubwa kwa wasichana wengi kuingia katika tabia hatarishi ambazo zinachangia kupata maambukizi.

“Zamani mazingira yalikuwa tofauti na sasa, mabinti walikuwa hawana simu janja na hivi sasa katika mitandao ya kijamii zinapatikana taarifa nzuri na mbaya.

“Changamoto kwa mabinti ni umasikini, wanakuwa hawana chanzo cha mapato, hivyo akiwa na matumizi mabaya ya mitandao ataanza kujilinganisha na wengine, atataka kuwa na mavazi mazuri, simu nzuri, kuonekana amesuka vizuri na matokeo yake anatumbukia kwenye hatari na kupata maambukizi,” anasema Dk Mwakyosi.

Anataja hatari nyingine kuwa ni uhusiano kati ya mabinti wadogo na wanaume waliowazidi umri ambayo mara nyingi inakuwa kwa lengo la kupata kitu.

“Kuna mabinti wanaingia katika mahusiano, ili kupata lifti za bodaboda au gari, chips kuku, bando, fedha au kupewa ufaulu. Akikutana na mwanaume anayempa fedha nyingi anajikuta hana uamuzi juu ya afya yake,” anasema.

Anataja changamoto nyingine ni mabinti kuona uhalali wa kuwa na wapenzi zaidi ya mmoja, jambo linalomweka hatarini zaidi.

Pia anaeleza kutopata elimu ya afya ya uzazi, kutojitambua kunamfanya binti ashindwe kufanya maamuzi sahihi katika mazingira hatarishi.

“Kuanza ngono mapema, wanakuwa katika hatari zaidi ya kupata maambukizi na ukatili wa kijinsia…tafiti zinaonyesha binti anapokaa shule kila mwaka kunampunguzia hatari ya kupata maambukizi,” anasema.

Dk Mwakyosi anasema tatizo ni kubwa nchini, hivyo umefika wakati wazazi wazungumze na mabinti zao, ili kupunguza maambukizi mapya.

“Tuachane na mila za zamani, mama na baba au walezi wakae na mabinti ili kuwaeleza taarifa sahihi wengi wanadhani wakifanya hivyo watamtuma akafanye, hiyo ni sahihi ni bora kumweleza kuliko aende akajigonga na kuanguka,” anasema Dk Mwakyosi ambaye ni daktari na mraghabishi wa masuala ya afya ya uzazi.

Dk Mwakyosi anasema ili kumsaidia binti inatakiwa kuwe na elimu na hata njia zinazopatikana kuzuia maambukizi ziendane na umri wao.

“Hauwezi kufananisha mabinti wa zamani na sasa, tunapaswa kukaa nao na kuwaeleza mbinu nzuri, taarifa muhimu na huduma muhimu. Kwanini tusifikirie kama nchi tukaamua zimfikie kila binti? Nchi tuweke bajeti ya kutosha katika huduma tofauti kusaidia mabinti wasipate maambukizi ya VVU,” anashauri.

Kutokana na takwimu za mambukizi ya VVU kwa wasichana kuongezeka, Dk Mwakyosi anasema huenda huduma zinazopatikana hazikidhi mahitaji yao kwa sasa, hivyo kuna haja ya kungalia zinazoendana nao.

Maambukizi ya VVU yanaenea kwa kasi zaidi kwa kundi la wasichana balehe wenye umri wa miaka 15-24 kwa asilimia 2.1 ikiwa ni mara tatu zaidi ya vijana wa kiume kwa asilimia 0.6.

Ongezeko la kundi hilo la wasichana balehe na wanawake vijana ambao ndiyo kinamama wa baadaye, linaipa mzigo mkubwa Serikali kuanza kujiandaa na namna itakavyozuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.

Ofisa ufuatiliaji na tathimini wa Tacaids, Nyangusi Laiser anasema asilimia 60 ya kundi balehe la vijana wenye umri kati ya miaka 15-24 walipima na kujua hali zao kwa mwaka 2020.

Anasema kati ya watu wanaioshi na VVU (WAVIU) wapya 68,000 mwaka 2020, asilimia 28 walikuwa na umri kati ya miaka 15 mpaka 24 na kati ya hao asilimia 67 walikuwa wasichana balehe na wanawake vijana huku wavulana wakiwa asilimia 23.

Anataja vyanzo vya maambukizi kwa kundi hilo ni pamoja na ndoa za kulazimishwa ambazo zinawaweka hatarini kupata mimba zisizotarajiwa, utoaji mimba na maambukizi ya magonjwa na zinaa na VVU.

“Wasichana wanaathirika zaidi kutokana na mila na desturi, mimba za utotoni, ngono za mapema, maambukizi ya magonjwa ya ngono, kutokuwa na maamuzi, unyanyasaji wa kijinsia na mengineyo,” anasema Nyangusi.

Anasema maambukizi mapya katika maeneo ya mjini ni asilimia 5.5 huku katika maeneo ya vijijini ni asilimia 4.2.

Nyangusi anasema kutokana na afua mbalimbali zinazotekelezwa nchini, idadi ya watu wanaofahamu kuwa wanaishi na VVU ni asilimia 84, asilimia 98 wanatumia ARV na asilimia 92 kati yao wamefubaza virusi hivyo.

Mwezeshaji wa masuala ya vijana, Florence Lema anashauri kila mmoja achukue jukumu lake kumlinda msichana.

Ni jukumu la walimu na wazazi kutoa elimu zaidi kwa kundi la wasichana balehe pamoja na wavulana, kwani hawawezi kuachwa nyuma, hii ni moja ya changamoto kubwa,” anasema.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments