TUNDU LISSU ATOA YA MOYONI MBELE YA RAIS SAMIA... ASHINDWA KUJIZUIA

 *Amuomba Rais atoe kauli ya kumkaribisha nchini yeye na wenzake


*Akumbusha mafao yake ya kulitumikia Bunge, awachongea akina Mdee

MJUMBE wa Kamati Kuu ya CHADEMA ambaye pia amewahi kuwa Mbunge wa Singida Mashariki kwa tiketi ya Chama hicho Tundu Lissu amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumpa fursa ya kuzungumza naye huku mambo mbalimbali huku akitoa ombi kwa Rais atoe kauli ya kumkaribisha nchini , kwani amechoka kukaa uhamishoni.

Akizungumza kupitia mitandao ya kijamii, Lussu amewaambia Watanzania amepata nafasi ya kutosha kuzungumza na Rais Samia , anamshukuru kwani mengi ambayo amemuelewa amekubali kuyafanyia kazi na jambo la kwanza ambalo amemuomba Rais ni kwamba afanye analoweza kuhakikisha kesi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe inaondolewa mahakamani kwani ni kesi ambayo amedai haina mashiko.

Nimemueleza Rais , kesi hii inayomkabili Mbowe inauzamiza Chama chake, inaumiza chama chetu , inamuumiza Mwenyekiti wetu, inaumiza familia yake, hivyo nimemuomba afanye analoweza kwa Mamlaka yake hii ksi iondolewe mahakamani, hakuna sababu ya kuwa na kesi ambayo kila mtu anaona ushahidi mahakamani mambo ya kuunga uunga tu na Rais ameahidi kushughulikia


Ajenda ya pili niliyozungumza na Rais na tumeizungumza kwa kirefu ni kuhusiana na suala la haki ya vyama vya siasa hasa vya upinzani vya kufanya shughuli za kisiasa kwa mujibu wa sheria bila vizuizi vilivyo nje ya sheria , nimemuomba Rais afute ili zuio haramu la vyama vya siasa vya upinzani kufanya mikutano ya hadhara pamoja na maandamano kama vile ambavyo sheria za Tanzania zinavyoruhusu.

Nimemwambia Rais kwamba ni suala la kuheshimu sheria za nchi yetu kama zilivyo ,sheria zinasema vyama vya siasa vinatakiwa kufanya mikutano ya hadhara na maandamano na vina haki ya kupatiwa ulinzi na jeshi la polisi pamoja na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kinapofanya mikutano na maandamano hayo na Mheshimiwa Rais amesema nalo atalishughulikia ,"amesema Lissu akielezea mazungumzo yake na Rais.

Wakati jambo la tatu ambalo wamelizungumza na Rais Samia linahusu Katiba mpya na mfumo mpya wa kidemokrasia ya uchaguzi kwa ajili ya nchi yetu."Nimemwambia Rais yeye anafursa ya kipekee na kihistoria ya kuipatia nchi yetu Katiba mpya na ya kidemokrasia, ana fursa ya kipekee na kihistoria ya kuhakikisha nchi inapata mfumo mpya wa kidemokrasia ikiwa pamoja na Tume huru ya uchaguzi.

Tuuhuishe sheria zetu za uchaguzi mbalimbali zitakazohakikisha kunakuwa na haki sawa kwa wote wanaoishiriki chaguzi, sheria ambazo zitahakikisha chaguzi zijazo zinakuwa huru na haki na tumezilingumza hili ikiwa ni ajenda yangu ya tatu, tumelizungumza kwa kirefu, nimemwambia mjadala wa Katiba mpya utakuwa mrefu lakini ni muhimu kama taifa tujadili suala hili muhimu,Rais amekubali kulishughulikia hili,"amesema.


Ameongeza kuwa jambo lingine ambalo wamelizungumza ni kuhusu yeye pamoja na wenzake ambao wamelizimika kuikimbia nchi kwasababu ya vitisho dhidi ya maisha yao."Kuhusu mimi mwenyewe nimemwambia Rais kwa vile ana mamlaka ya kuhakikisha sasa ninapata haki zangu nilizonyimwa baada ya kushambuliwa ,haki ya kupatiwa matibabu kwa mujibu wa sheria.

Nimemwambia Rais na kumuomba kwa vile ana mamlaka hayo ashughulikie suala hilo na amelichukua , nimezungumza na rais kuhusu mazingira yote ya kuondolewa kwangu bungeni Juni mwaka 2019 na kutolipwa kiinua mgongo kinyume na sheria husika za nchi yetu, nimemueleza Rais kwamba mimi mbunge pekee wa Bunge lililopita ambaye sikulipwa mafao yangu na Rais amenidokeza aliambiwa na spika siwadai chochote.

Kwa hiyo mheshimiwa Rais amesema hilo atalishughulikia na nimemshukuru kwa hilo, nimemwambia Rais ninahitaji kurudi nyumbani kama ambavyo nilishatangaza siku za nyuma, kukaa uhamishoni ni kukaa uhamishoni tu, ninapenda kurudi nyumbani , na kwasababu ya mazingira niliyoondokea Tanzania ninahitaji yeye kama Rais wa nchi yetu atoe kauli ya kunikaribisha nyumbani

Atoe kauli ya kunitoa wasiwasi kwamba nikirudi nyumbani ninaweza nikadhuriwa, aseme ananikaribisha nyumbani na nitakuwa salama , hicho tu na Rais amesema hilo atalifanyia kazi na amekubali, vile vile kuhakikisha ninapata hati ya kusafiria kwasababu hati yangu ya kusafiria iliibiwa nikiwa Ujerumani.

Pia nimezungumza kwa niaba ya Godbless Lema na Ezekia Wenje ambao nao wako uhamishoni Canada na nimemuomba Rais kama ilivyo kwangu Lema na Wenje walikimbia nchi kwasababu ya vitisho dhidi ya maisha yao na nimemuomba atukaribishe na kutupa uhakika vitisho havitakuwepo na tutakuwa salama na Rais amesema atalifanyia kazi".

Wakati huo huo, Lissu amesema pia wamezungumza na Rais kuhusu wabunge 19 wa Spika Ndugai na sasa ni wabunge wa Dk.Tulia Ackson"Nimemwambia Rais waleo si wabunge wa Chadema tulishawafukuza uwanachama , kwasababu hiyo na kwa mujibu wa Katiba yetu ambaye si mwanachama wa chama cha siasa hastahili kukaa bungeni kulipwa fedha za umma wakati hana sifa ya kukaa bungeni.

"Haijalishi kuna rufaa ,suala la rufaa ni tofauti kabisa, kwa sasa sio wanachama wa Chadema, kuendelea kuwalipa fedha za umma ni kufanya ufujaji wa fedha za umma, nimemuomba rais ashughulikie hilo.Ajenda ya tano nimemwambia Rais kwamba atuongeze, yeye ni Rais wetu wote na kwasababu ni Rais anajukumu la kipekee la kutuongoza katika kuiponya nchi yetu , nimemueleza Rais wetu nchi yetu ina makovu mengi, ina maumivu mengi , ina vilio vingi

Watu wengi wameumizwa katika miaka sita kuanzia 2015 , nimemwambia Rais ni yeye mwenye jukumu na fursa ya kuisaidia nchi yetu kuponya majereha yote, kuponya vilio vyetu hivi , kufuta machozi wote ambao wanalia nimemwambia Rais afanye hiyo kazi na moja ya kuifanya hiyo kazi ni kutekeleza ahadi yake aliyoitoa bungeni wakati anahutubia mara ya kwanza kwamba atakutana na viongozi wa vyama vya upinzani.

Nimemwambia Rais watanzania watafurahi, marafiki zetu wa kimataifa watafurahi.Hata hivyo Rais amefanya jambo la maana sana kunipa fursa ya kuzungumza naye haya , tunafahamu ,nafahamu kuwa kuna mambo mengi yanahitaji yajadiliwe na sisi tuko tayari kuendelea na majadiliano ya masuala yote ambayo yanatatiza kama Taifa letu, tuko tayari kushirikiana naye katika mambo yote yanayohitaji kuwekwa sawa, raisa amefanya jambo jema na amenipa fursa ya kueleza haya."amesema Lissu.


Post a Comment

0 Comments