Mkutano wa Umoja Mataifa wa kujadili madhara ya plastiki wafanyika Nairobi

Mkutano wa mazingira wa Umoja wa Mataifa umeanza Jumatatu mjini Nairobi Kenya kwa lengo la kujadili mkataba wa kimataifa wa kupunguza utumizi wa plastiki zinazoharibu mazingira.

Kwa mujibu wa taarifa, wawakilishi wa nchi zaidi ya 100 wanatazamiwa kuafikiana kuhusu mkataba wa kwanza wa kimataifa kuhusu taka za plastiki katika kikao hicho cha siku tatu ambacho kinafanyika ana kwa ana na kwa njia ya intaneti.

Akizungumza wakati wa ufungui, Rais wa Mkutano wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa (UNEA) Inder Andersen amesema dunia sasa ina fursa ya kuandika ukurasa mpya katika historia kwa kuanzisha mkakati wa pamoja wa kukabiliana na tatizo sugu la taka za plastiki.

Andersen amesema umma unaunga mkono hatua za kukabiliana na tatizo la plastiki katika mazingira na hivyo washirki wa mkutano wanatakiwa kutekeleza majukumu yao.

Mwanaharakati nchini Kenya akiwa amebeba bango la kuunga mkono marufuku ya plastiki

Wanaharakati wa mazingira wanataka mkataba ambao utashughulikia suala la uchaguzi wa mazingira utokanao na mfumo mzima wa uzalishaji plastiki hadi matumizi. Erastus Ooko wa harakati ya kulinda mazingira ya Greenpeace Africa anasema taka za plasitki ni sawa na bomu linalokaribua kulipuka na hivyo hakuna budi ila kuchukua hatua za lazima za kukailiana na tatizo hilo.

Baadhi ya nchi duniani tayari zimeshapitisha miswada ya  kupiga  marufuku vitu vinavyochangia uharibifu wa mazingira ikiwemo matumizi ya bidhaa za plastiki ili kukomesha uchafuzi wa mazingira ya miji na ya bahari utokanao na matumizi ya plastiki.

Mwaka 2017, Kenya iliidhinisha marufuku dhidi ya matumizi ya mifuko ya plastiki nchini. Hatahivyo uchunguzi uliofanyika hivi karibuni umebaini kuwa mifuko ya plastiki bado inauzwa kwa siri hata baada ya kupigwa marufuku.

 

Post a Comment

0 Comments