WIZARA YA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA YAELEZA MAFANIKIO YA MWAKA MMOJA KATIKA SERIKALI YA AWAMU YA SITA

SERIKALI kupitia Wizara ya Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa katika kipindi cha mwaka mmoja wa awamu ya sita imeingia kwenye mafanikio mengi ikiwemo kutatua migogoro ya ardhi 74 Mkoani Arusha ambayo inahusisha maeneo ya jeshi na wananchi.

Hayo yameelezwa leo Jijini hapa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa Dkt.Stergomena Tax katika kikao chake na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya kipindi cha mwaka mmoja wa Serikali ya awamu ya sita tangu Rais Samia Suluhu Hassan aliposhika madaraka ya kuiongoza Tanzania.

Amesema,Licha ya changamoto zilizojitokeza kwenye baadhi ya maeneo ,Wizara hiyo imeendelea kuwa kinara kwenye utoaji mafunzo ya kijeshi katika Vyuo na shule za kijeshi ndani na nje ya nchi,utoaji mafunzo ya awali ya kijeshi kwa vijana wa JKT na utoaji huduma za matibabu kwa wanajeshi na familia zao ,vijana wa JKT,watumishi wa Umma na wananchi

"Tunaendeleea kustawi pia katika uhawilishaji wa Teknolojia kwa ajili ya kuzalisha mazao ya msingi,udumishaji wa ushirikiano kitaifa na kimataifa katika sekta ya ulinzi,utatuzi wa migogoro ya ardhi,ujenzi wa makao makuu ya ulinzi wa taifa na utoaji wa kipaumbele katika uendelezaji miradi ya kielelezo na kimkakati na ulipaji madeni ya wazabuni waliotoa huduma mbalimbali,"amesema.

Ameeleza kuwa kama lilivyo jukumu la Wizara hiyo katika kulinda Taifa dhidi ya maadui toka ndani na nje ya nchi,itahakikisha nchi inakuwa salama na kulinda amani ikiwa ni pamoja na kuimarisha mshikamano baina yake na wananchi wake.

Amesema,Kwa kipindi cha mwaka mmoja, Serikali imeiwezesha Wizara hiyo kutekeleza majukumu yake ya msingi kwa weledi,umakini na mafanikio hivyo kuwezesha nchi kuendelea kuwa na amani na utulivu ikiwa ni pamoja na kulipa madeni yenye thamani ya zaidi ya shilingi Bilioni 175 Kwa wazabuni waliotoa huduma mbalimbali.

"Hii imejenga imani kwa Serikali na kuiwezesha Wizara kuendesha majukumu yake ya msingi kwa ufanisi,na tutaendelea kusimama zaidi katika kulinda amani ambapo wizara hii kupitia JWTZ inaendelea kuondoa changamoto chache katika baadhi ya mipaka hususani Kusini na hivyo tupo salama,"amefafanua Waziri huyo .

Pia amesema Serikali imeendelea kudumisha ushirikiano wa kimataifa na kitaifa kupitia sekta ya ulinzi hususani kushirikiana na umoja wa mataifa (UN),Umoja wa Afrika(AU)na Jumuiya ya maendeleo Kusini mwa Afrika(SADC)katika operesheni mbalimbali za Ulinzi wa amani kwa kupeleka vikosi na usaidizi,waangalizi wa Jeshi na makamanda katika nchi zenye migogoro.

"Chini ya Serikali ya awamu ya sita , JWTZ linavyo vikosi vya Ulinzi wa amani katika nchi za Lebanon,Jamhuri ya kidemokrasia ya watu wa Kongo na Jamhuri ya kati,Jeshi hili pia linashiriki katika kamisheni ya SADC (SAMIM)katika kupambana na ugaidi huko Msumbiji,"ameeleza

Hata hivyo ameeleza kuwa ili kuwa na Taifa imara , Serikali imeendelea kutoa mafunzo ya awali ya kijeshi kwa vijana wa mujibu wa sheria na vijana wa kujitolea kwa lengo la kujenga uzalendo na ukakamavu ikiwa ni pamoja na kutekeleza miradi adhima ya kuwajengea vijana stadi na uwezo wa kujitegemea.

Pamoja na hayo amesema Serikali kwa kutambua umuhimu wa afya bora Kwa wanajeshi wao,Wizara imeendelea kutoa huduma za matibabu Kwa maofisa ,askari,vijana wa JKT na Watumishi wa Umma na familia zao na kuona umuhimu wa kuwajengea makazi bora yenye hadhi ili kutekeleza majukumu yao Kwa ufanisi.
Na Zena Mohamed,Dodoma.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments