HATIMAYE kwa mara ya kwanza Msaanii wa muziki wa kizazi kipya Zuhura Othman Soud a.k.a Zuchu pamoja na Mwanadada anayetesa kwenye muziki huo Faustina Charles Mfinanga maarufu kwa jina la Nandy wamejikuta wakiwa kwenye jukwaa moja la Chama Cha Mapinduzi ( CCM) walipokuwa wakitoa burudani kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum wa Chama hicho waliokutana Leo Aprili 1 Mjini Dodoma.
Kwa kukumbusha tu tangu Zuchu aingie kwenye muziki wa Bongo Fleva na kutikisa kwa nyimbo zake mbalimbali hajawahi kuwa jukwaa moja na Nandy ambaye yeye kwenye muziki huo anajulikana kwa jina la Malkia na amekuwa kwenye muziki huo kwa muda mrefu kuliko Zuchu.
Wasanii hao ambao kila mmoja amejizolea mashabiki wake na wakati mwingine Watanzania wanaowafuatilia wasanii kuanza kutafuta nani ni zaidi ya mwingine.Kwa nyakati tofauti wasanii hao wamekuwa wakiandaa matamasha na wakati mwingine kushirikishwa kwenye kazi za wasanii wengine lakini hawajawahi kukutana jukwaa moja na kiu ya walio wengi ilikuwa kuona siku moja wanakutana kwenye steji moja.
Kupitia CCM leo Nandy na Zuchu wamejikuta wakipanda jukwaani kutoa burudani kwa wajumbe hao ambao waliokuwa wakiongozwa na Mwenyekiti wa Chama hicho na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.
Kwa mujibu wa ratiba ya burudani kwenye mkutano huo, Zuchu alikuwa wa kwanza kupanda jukwaani kuonesha manjonjo yake ya kuimba kwa sauti yake laini huku yakinogeshwa na unenguaji wake alikonga nyoyo za Wana CCN waliopo kwenye mkutano huo na wale wanaofuatilia kupitia luninga na redio zinazorusha mkutano huo .
Baada ya Zuchu kumaliza kutoa burudani baadae ikafuata zamu ya Nandy ambaye naye alikuwa amejiandaa vilivyo.Akatumia nafasi hiyo kuthibitisha yeye ndio yeye, akatawala jukwaa kwa nyimbo zake mbalimbali ukiwemo wimbo Maalum aliotunga kwa ajili ya mkutano mkuu Maalum wa CCM.
Kualikwa kwa wasanii hao kwenye mkutano huo angalau unakwenda kutuliza mzuka wa mashabiki wao baada ya kuwaona wakitoa burudani kwenye jukwaa moja.
0 Comments