Afrika Kusini: Kuanzia sasa watoto hawatohitajika tena kuvaa barakoa kujikinga na corona


Serikali ya Afrika Kusini jana Alkhamisi iliondoa ulazima wa watoto kuvaa barakoa wanapokuwa mashuleni licha ya kuweko taarifa kuwa maambukizo ya ugonjwa wa corona yameongezeka nchini humo. Tarehe ya mwisho ya wajibu wa kuvaa barakoa wanafunzi madarasani ilimalizika usiku wa kuamkia jana na haikuongezewa muda.

Hata hivyo watu wazima wanatakiwa waendelee kuvaa barakoa wanapokuwa maeneo ya ndani ya umma huku idadi maalumu ya watu wanaotakiwa kushiriki kwenye matukio yoyote ya pamoja ikiendelea pia kuhimizwa nchini humo.

Takwimu rasmi za serikali ya Afrika Kusini zinaonesha kuwa watu milioni 3.8 wamekumbwa na ugonjwa wa UVIKO-19 nchini humo huku idadi ya waliofariki dunia ikiripotiwa kuwa ni watu 100,407. Idadi hiyo ni kubwa zaidi katika bara zima la Afrika. Sasa hivi zaidi ya asilimia 45 ya watu wazima wameshapiga chanjo kamili ya corona nchini Afrika Kusini.

Raia wa Afrika Kusini akipiga chanjo ya corona

Wizara ya Afya ya nchi hiyo imesema, njia pekee ya kuweza kujikinga na corona sisi wenyewe na wapendwa wetu, ni kuongeza idadi ya waliopiga chanjo na kuheshimu hatua zote za kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo kuliko wakati mwingine wowote.

Baada ya kupungua kidogo maambukizi ya corona mwezi uliopita idadi ya watu waliokumbwa na ugonjwa huo ilipanda tena juzi Jumatano. Zaidi ya wagonjwa wapya 6,100 wa corona waliripotiwa nchini Afrika Kusini.

Idadi ya watu wanaoruhusiwa kukusanyika pamoja katika maeneo ya ndani nchini humo mwisho ni 1,000 au nusu ya idadi yoyote ya watu wanaoweza kuingia kwenye eneo husika la ndani lililofungwa kila upande.


 

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments