Migogoro ndani ya vyama Inavyovuruga demokrasia

Wakati Tanzania ikielekea kutimiza miaka 30 tangu mfumo wa vyama vingi urejeshwe hapa nchini mwaka 1992 na kushuhudia Uchaguzi Mkuu wa kwanza uliohusisha vyama hivyo mwaka 1995, bado migogoro ndani ya vyama vya siasa, husasan vya upinzani imekuwa kikwazo na kurejesha nyuma harakati za kukuza demokrasia.

Kimsingi migogoro hiyo imekuwa na picha tofauti ndani na nje ya vyama hivyo, wapo wanaoona uwepo wake ni kuonyesha vyama husika havina ukomavu na uvumilivu wa kisiasa, lakini wapo pia wanaoona kuna mingine hupandikizwa na watawala kuvivunja nguvu.

Mara kwa mara vyama vilivyo na nguvu na vinavyoonekana kuwa tishio kwa chama tawala ndivyo vimekuwa vikibaliwa na migogoro ya kuwania uongozi, matumizi ya fedha au mgawanyo wa rasilimali walizonazo.

NCCR-Mageuzi

Chama cha National Convention for Construction and Reform (NCCR-Mageuzi), kipo kwenye mnyukano wa haja. Ugomvi ni uongozi.

Joseph Selasini, akisoma maazimio ya Halmashauri Kuu ya chama hicho, alisema Mwenyekiti James Mbatia na Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara, Angelina Mtahiwa, wamesimamishwa.

Baadaye, Katibu Mwenezi wa chama hicho, Edward Simbeye aliwaambia waandishi wa habari kuwa kilichotangazwa na Selasini ni uhaini ndani ya chama.

Halafu Simbeye alisema kuwa kabla ya tukio la Selasini kutangaza kusimamishwa kwa Mbatia na Angelina, tayari walikuwa wameshawasilisha barua Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, kuhusu uamuzi wa Kamati Kuu ya NCCR-Mageuzi kumsimamisha kazi Katibu Mkuu, Martha Chiomba.

Kabla ya taarifa ya Simbeye, Martha alifika Makao Makuu ya NCCR-Mageuzi, akafunga ofisi zote, akasema hakuna shughuli yoyote ambayo ingefanyika. Martha aliondoka na funguo.

Simbeye alifika baadaye. Ujio haukuwa wa amani. Ulitokea mnyukano wa kimwili hadi kushikiana mawe na matofali. Kisha, Simbeye akatangaza kuirejesha ofisi katika mikono salama.

Haukupita muda mrefu tangu Simbeye azungumze na vyombo vya habari, Mbatia aliwasili Makao Makuu ya NCCR-Mageuzi, akiongozana na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Zanzibar, Haji Ambar Khamis. Hawakuzungumza chochote.


Unapata picha gani?

Mkutano wa Halmashauri Kuu NCCR-Mageuzi ulibarikiwa mpaka na Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza. Kauli ya Nyahoza ni kwamba Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ilipokea barua kutoka Halmashauri Kuu ya NCCR-Mageuzi ikiwajulisha kuhusu mabadiliko.

Kwa mujibu wa Nyahoza, mabadiliko ambayo yalitajwa kwenye barua ya Halmashauri Kuu ya NCCR-Mageuzi ni kuvunjwa kwa bodi ya wadhamini, vilevile kuwasimamisha kazi Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara.

Mpaka hapo unabaini kuwa Halmashauri Kuu ya NCCR-Mageuzi, ina nyota wake wa mchezo ambaye ni Selasini na Martha Chiomba. Kama utaipitia historia ya NCCR-Mageuzi kwa vizazi kadhaa nyuma, utamweka pembeni Martha, utabaki na Selasini. Huyo ndiye nyota wa mchezo wa Halmashauri Kuu.

Sasa, Halmashauri Kuu ya NCCR-Mageuzi chini ya Selasini, ina mawasiliano ya moja kwa moja na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa. Liweke hilo kichwani.

Rejea taarifa ya Selasini. Alisema Halmashauri Kuu NCCR-Mageuzi imemwagiza Katibu Mkuu, Martha Chiomba, aivunje sekretarieti ya chama hicho. Hapo unapata tafsiri kuwa Selasini na wenzake wanataka kuubadili uongozi wote wa NCCR-Mageuzi.

Tuje upande wa pili, Simbeye alisema kuwa Kamati Kuu chini ya Mbatia iliwasilisha barua Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, kueleza uamuzi wa kumwondoa Katibu Mkuu (Martha Chiomba).

Kumbe sasa, Kamati Kuu ya NCCR-Mageuzi chini ya Mbatia na Halmashauri Kuu inayoongozwa na Selasini, kila upande una mawasiliano na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.

Mwisho kabisa, unapata jawabu lililonyooka kuwa ndani ya NCCR-Mageuzi, kuna vita ya mafahari wawili; Mbatia na Selasini


Ni sinema kubwa

Mbatia na Selasini walikuwa vijana kipindi NCCR-Mageuzi inaanzishwa mwaka 1992. Na walihusika kwenye vuguvugu la mageuzi tangu mwaka 1990.

Mwaka 2009, Selasini alihama NCCR-Mageuzi, akajiunga na Chadema, alikopewa tiketi ya kugombea ubunge jimbo la Rombo. Akashinda.

Maisha ya Selasini Chadema yalikuwa ya miaka 11. Mwaka 2020, Selasini alirejea NCCR-Mageuzi. Miaka miwili baadaye, ameibuka na maazimio ya kumwondoa Mbatia kwenye chama.

Kwa nini ni sinema? Mwaka 2009 wakati Selasini anaondoka NCCR-Mageuzi kwenda Chadema, hoja kubwa ni kwamba alitofautiana na Mbatia.

Swali; mgogoro wa sasa kati ya Mbatia na Selasini ni kisasi cha miaka mingi au kweli kuna matatizo mapya ambayo wameshindwa kuyapatia ufumbuzi.

Je, Selasini alirejea NCCR-Mageuzi kwa sababu ya kuona hakukuwa na maelewano Chadema, au alirejea kumshughulikia Mbatia baada ya kuwa amejipanga upya?


Msuli wa Mbatia

Mbatia yupo NCCR-Mageuzi tangu chama hicho kilipoanzishwa. Alikuwa kijana mno akiwa mmoja wa waasisi wa chama hicho.

Chama hicho kimepitia hekaheka nyingi lakini Mbatia amebaki imara. Akiwa bado kijana, Mbatia alichomoza katikati ya mgogoro wa uongozi, uliowahusisha aliyekuwa Mwenyekiti, Augustino Mrema na Katibu Mkuu, Mabere Marando.

Kumbukumbu kubwa ni mwaka 1997, kwenye Hoteli ya Raskazone, Tanga. Wafuasi wa Mrema na Marando walinyukana. Mrema aliokolewa na mlinzi wake, Mohammed Posh.

Mrema aliondoka na kwenda kujiunga na Tanzania Labor Party (TLP), Marando akakosa nguvu. Tayari Mbatia alishajiimarisha kupitia mgogoro wa Marema na Mbatia.

Mwaka 1999, ulifanyika uchaguzi mkuu NCCR-Mageuzi, Marando aligombea uenyekiti dhidi ya Mbatia, ambaye alimgaragaza mwanasheria huyo mkongwe nchini.

Historia ya NCCR-Mageuzi inaonesha kuwa Mbatia ni mfupa mgumu uliowaondoa kwenye reli wanasiasa wakubwa nchini. Marando ni mmoja wao, mwingine ni wakili maarufu na mbunge wa zamani wa jimbo la Ubungo, Masumbuko Lamwai. Zingatia kuwa Lamwai ni kaka wa damu wa Selasini.

Katika vijana wa NCCR-Mageuzi zamani, yupo pia Anthony Komu, ambaye baadaye alihamia Chadema. Komu na Selasini walirejea NCCR-Mageuzi mwaka 2020. Na katika hili, Komu yupo na Selasini. Je, ni misheni ya pamoja?

Mwaka 2011, aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila alianzisha vuguvugu la kumwondoa Mbatia kwenye uenyekiti. Hata hivyo Kafulila aliishia kufukuzwa uanachama. Ingawa alikimbilia mahakamani kuomba zuio la kufukuzwa uanachama, baadaye aliketi na Mbatia wakayamaliza.

Hata mwaka 2015, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Tanzania Bara, Leticia Mosore alijaribu kuupima ubavu wa Mbata lakini aliangukia pua.

Je, safari hii Selasini kwa kuungwa mkono na Komu, Martha Chiomba na Halmashauri Kuu, wataweza kumwondoa Mbatia, au Injinia huyo aliyefukuzwa Chuo Kikuu Dar es Salaam kwa sababu ya harakati, ataendelea kuwa mfupa mgumu?



Taswira ya mageuzi

NCCR-Mageuzi wanaingia kwenye mnyukano kipindi ambacho vyama vingine vilivyopo kwenye kundi la upinzani, navyo vinasuguana.

Mathalan, sasa hivi Chadema wanavutana kuhusu suala la wabunge 19 ambao chama hicho kinadai walikwenda bungeni na kuapishwa bila ridhaa ya uongozi wa juu.

Wabunge hao 19, walifukuzwa uanachama kwenye mkutano wa Kamati Kuu wa Novemba 2020. Walikata rufaa, kisha Baraza Kuu likakazia uamuzi wa Kamati Kuu.

Chadema bado mambo hayajawa sawa na NCCR-Mageuzi umeibuka mgogoro ukiwa haujapita muda mrefu tangu ACT-Wazalendo wamalize uchaguzi wa kujaza nafasi ya Mwenyekiti.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Seif Sharif Hamad, alifariki dunia Februari 17, 2021. Chama hicho kilipitisha takriban mwaka mmoja bila kuwa na mwenyekiti. Kisha, wakafanya uchaguzi, Juma Duni Haji akashinda.

Polisi wakiwatuliza madiwani wa Chadema na CUF baada ya kutokea ghasia wakati wa uchaguzi wa Naibu Meya wa Ilala uliofanyika jana katika Ukumbi wa Arnatoglo, jijini Dar es Salaam. Katika uchaguzi huo Mgombea wa CCM, Omar Kumbilamoto alitangazwa kushinda uchaguzi kwa kura 25 dhidi ya 25 alizopata mgombea wa CUF. Picha na Omar Fungo

Baada ya Duni kushinda, hali ikawa si shwari ndani ya ACT-Wazalendo. Wanachama waandamizi wakakimbilia Chama cha Wananchi (Cuf). Hivyo, ACT walimeguka.

Wakati huohuo, Cuf (Civic United Front), ndicho chama kilichokuwa kinaongoza mwendo wa upinzani Zanzibar. Mambo yaligeuka Machi 18, 2019, Seif alipotangaza kuhama Cuf na kujiunga na ACT-Wazalendo. Viongozi wengi waliokuwa Cuf pamoja na wanachama, walihama naye. Hata wabunge waliokuwa Cuf, wote, mara Bunge lilipovunjwa, walihamia ACT.

Utapata tafsiri kuwa waliohama ACT-Wazalendo kwenda Cuf ni kama wanarejea nyumbani. Je, wanataka kuimarisha nyumba ya zamani na kumoboa mpya?

Katika maisha ya kisiasa, hakuna wakati unaona wana-CCM wanaondoka kwenye chama kwa sababu ya kushindwa uchaguzi wa ndani. Hutokea katika kutafuta nafasi ya kugombea uongozi wa urais, ubunge na hata udiwani. Anayeshindwa CCM anakwenda upinzani kutafuta fursa.

Wapinzani wao, mara nyingi watu huhama kwa kushughulikiana. Mwenye nguvu anawafundisha adabu wanyonge. Migogoro inakuwa mingi, hivyo kudhoofisha mageuzi.

Cuf yenye Prof Ibrahim Lipumba na Maalim Seif, iliwapoteza wanachama wengi, wakiwemo viongozi wa ngazi za juu kabisa. Profesa Abdallah Safari alihamia Chadema kutoka Cuf. Wilfred Lwakatare alihamia Chadema pia. Hawa walikuwa viongozi waandamizi.

Safari na Lwakatare ni mfano mdogo kuonesha kuwa baada ya uchaguzi wa ndani, kwa historia ya Tanzania, vyama vya upinzani huwa havibaki salama asilimia 100. Migogoro ni uongozi.

Desemba 2019, Chadema waliondokewa na wanachama wao wengi tu, tena waandamizi na waliokuwa viongozi. Walinung’unika kuminywa kwa demokrasia ndani ya chama.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Kanda ya Pwani, Frederick Sumaye, Mwenyekiti wa Kanda ya Kusini, Cecil Mwambe, vilevile Profesa Safari, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Chadema, walijiondoa kwenye chama hicho. Mwambe na Sumaye walielekea CCM, Safari hajaeleweka.

Uchaguzi wa ndani ACT-Wazalendo mwaka 2020, ulipomalizika kuna ambao walitimka. Mmoja wao ni Jeremiah Maganja, aliyekuwa Kaimu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo. Maganja alihamia NCCR-Mageuzi, alikosimama kama mgombea urais kwenye Uchaguzi Mkuu 2020.

Kuna historia ya mapinduzi, Aman Jidulamabambasi alimshughulikia Mwenyekiti wa United Democratic Party (UDP), John Cheyo, ingawa mapinduzi yalizimwa. Hata Mrema aliwahi kupinduliwa lakini akayashinda mapinduzi.

Hivyo, mgogoro wa NCCR-Mageuzi, Chadema na historia za migogoro kwa vyama vyote vya upinzani, hutoa istana mbaya kwao kuwa hawajapevuka kiasi cha kutosha kushika dola. Kama wao kwa wao wanavurugana kila mara, nchi wataiweka salama kweli?

 

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments