Majaliwa: Tutatekeleza maagizo ya Shaka

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema maagizo na maelekezo yote ambayo yametolewa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka yatatekelezwa na watumishi wote wa umma Mkoa wa Lindi.

Kauli hiyo ameitoa leo Jumatano Juni Mosi 2022 mkoani Lindi wakati Shaka akihitimisha ziara yake ya siku nne aliyoifanya ambapo Waziri Mkuu amesema hakuna agizo moja ambalo hatatekelezwa.

“Umekutana na wananchi wa Mkoa wa Lindi, umetembelea miradi ya maendeleo, sisi wana Lindi tumefurahi sana kupata taarifa yako ya mafanikio ambayo yamepatikana, umewapongeza watumishi wa umma, nataka kukuhakikishia nami nilifanya ziara kwenye wilaya zote za mkoa huu, nimepata kutembelea miradi.

“Ulichokiona wewe nami ndicho nilichokiona watumishi hawa ndio wanaotekeleza miradi hiyo. Mkoa wa Lindi kuna mabadiliko na hizi ni jitihada zinazofanywa na Chama Cha Mapinduzi kupitia Serikali yetu inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan,” amesema Waziri Mkuu.

Amefafanua kuwa taarifa ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM imeeleza kwa kina kuhusu mafanikio yaliyopatikana kwenye Mkoa wa Lindi huku akitumia nafasi hiyo kueleza kuwa katika miudombinu ya barabara, tayari Serikali imeweka mipango ya kujenga barabara mbalimbali za mkoa huo.

“Barabara zetu ikiwemo ya Masasi, Nachingwea mpaka Liwale imeshaingia kwenye mpango wa utafutaji fedha na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi ameshaiweka kwenye mipango ya ujenzi, hivyo kinachosubiriwa ni kupata fedha.

“Umezungumzia kuhusu wanyamapori nami nimepokea, Mbunge wa Nchingwea Dk Amandus Chinguile alikuja mezani kwangu bungeni kunieleza, nilimuagiza Waziri apite huku Liwale, Nachingwea na maeneo mengine ya Lindi hadi kule maeneo ya Milola, Naibu Waziri alikuja amepita na ameona.

“Tunakwenda kuona idadi ya mifugo iliyoingia Selous idhibitiwe ili tembo warudi, tembo hawakubali kuchanganyika na mifugo mingine, hivyo tembo wale wanasogea huku Serikali itasimamia hili na bahati nzuri Naibu Waziri alikuja na akaongazana na mbunge wa Nachingwea, hivyo tutahakikisha tunatekeleza maagizo yako ili kudhibiti wanyampori ambao wanakuja kwenye maeneo ya watu,’ amesema Waziri Mkuu.

Kuhusu fidia kwa walioathiriwa na tembo, Waziri Mkuu amesema malipo yao yanaendelea kujadiliwa na wanaostahili kupata fidia kutokana na athari ambazo wamezipata kutokana na tembo hao zitawafikia.

“Katika Bunge hili la Bajeti Wizara ya Maliasili na Utalii itasoma bajeti yake na hili la fidia litakuwepo , hivyo wanaostahili fidia watalipwa,’amesisitiza Waziri Mkuu

 Kuhusu bei ya mazao mbalimbali likiwemo zao la ufuta, Waziri Mkuu amesema Serikali imefanya utaratibu mzuri wa kupanga bei na hivi sasa wameshuhudia bei mpya kwenye mazao ikianza kunufaisha wakulima

Ametolea mfano kuwa wakulima wa Namtumbo wameanza kunufaika na mfumo huu unatokana na utaratibu wa stakabadhi ghalani ingawa wakati unaanza kuna watu waliupinga na kuna baadhi ya wanasisa waligeuza kuwa ni suala la kisiasa.

Akizungumzia agizo la Shaka la kuitaka Serikali kuangalia namna ya kupunguza makato ya ushuru kwenye zao la ufuta ili wakulima wanufaike, Waziri Mkuu amesema agizo hilo watalifanyia kazi na tayari Rais Samia Suluhu Hassan ameshampa jukumu la kupitia makato na ameanza kuzunguka kila mkoa kwenye zao ambalo linanufaisha wakulima.

“Napita kuangalia makato, ninyi ni mashahidi nilipokuwa Kagera kulikuwa kuna makato 47 lakini tumeyapunguza. Serikali inataka kuona mkulima huyu anayevuja jasho ananufaika na kilimo, hivyo suala la makato tunalifanyia kazi na hakuna mzaha kwenye hili,”amesema.

Awali akizungumza wakati wa majumuisho hayo, Shaka ameeleza kwa kina kuhusu mafanikio ambayo ameyashuhudia kwenye Mkoa wa Lindi na hiyo imetokana na upendo mkubwa alionao Rais Samia Suluhu Hassan kwa wakazi wa Lindi na Watanzania.

“Katika Mkoa wa Lindi nimepita kila mahali kunajengwa, barabara zinajengwa, vituo vya afya, shule na majengo mengine ya huduma za kijamii yanaendelea kujengwa .Serikali imetoa zaidi ya Sh52 bilioni kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo,”amesema Shaka.

Amesema pamoja na mafanikio ya mkoa huo, bado kuna changamoto ya wanyamapori hata tembo kuvamia makazi ya watu na mashamba na hivyo kuleta athari zikiwemo za kujeruhi watu na kusabisha vifo, kuharibu hivyo ameitaka Serikali ichukue hatua kukabiliana na tembo hao.

Pia ametoa maelekezo kwa Serikali kuangalia namna ya kupunguza ushuru katika mazao kwani pamoja na bei ya ufuta kuongezeka kutoka Sh2100 hadi Sh2900 lakini mkulima hapati fedha yote hiyo kwasababu ya ushuru uliopo.

 

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments