Wagombea CCM Moshi waonywa kukiuka utaratibu

CCM Wilaya ya Moshi vijijini, mkoani Kilimanjaro kimewaonya makada wake walioomba nafasi za uongozi ndani ya chama hicho, kuacha kufanya kampeni katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi na kwamba hawatasita kuwachukulia hatua wale watakaobainika kwenda kinyume cha kanuni za uchaguzi.

Rai hiyo imetolewa leo Ijumaa Septemba 16, na katibu wa CCM Wilaya ya Moshi Vijijini, Ramashan Mahanyu wakati akizungumza na wajumbe wa Halmashauri kuu pamoja na wagombea katika Wilaya hiyo.

Katibu amesema tayari wameteua timu itakayokwenda kusimamia uchujaji wa majina ambao unaanza leo septemba 16 kwenye Eilsya hiyo na kwamba haki itatendeka kwa kila mmoja.

“Tunahitaji viongozi ambao watakisemea chama vizuri na kukivusha katika uchaguzi wa serikali za mitaa 2024 na uchaguzi mkuu 2025 na ni vyema wagombea wakatambua kuwa, kugombea ni kitu kingine na kuteuliwa ni kitu kingine.

“Lakini pia naomba wote mtambue kuwa sisi kama viongozi wa chama hatuna mgombea, wote ni wagombea wa chama na nitamshangaa katibu kata atakayeitisha mkutano kwa ajili ya mgombea fulani,” amesema.

Aidha katibu huyo ametangaza ratiba ya uchaguzi itaanza Septemba 23 kwa Umoja wa Vijana (UVCCM), Semptemba 24 Umoja wa Wanawake (UWT) na Septemba 25 itakuwa ni Jumuiya ya Wazazi.

Kwa upande wake mwenyekiti wa CCM katika Wilaya hiyo, Cyril Mushi amewataka wanachama wa chama hicho, katika kuelekea kwenye uchaguzi wa chama, kukubali katika ushindani kwa kuwa ni lazima mmoja ndiye atashinda.

"Kwa sasa vyama vya siasa ni vingi na ushindani utakuwa mkubwa hivyo viongozi watakaopatikana hawatakiwi kuwa legelege, wanatakiwa kuwa na maono na wenye kukipenda chama na wenye hoja za kisiasa zitakazowezesha kushindana na upinzani," amesema.

Aidha amesema katika kipindi cha miaka mitano akiwa madarakani, anajivunia kuimarisha umoja ndani ya chama, kupata hatimikiki ya maeneo ya chama na katika kipindi cha mwezi mmoja.

“Tumesajili zaidi ya wanachama 6,500 katika mfumo wa kielektroniki  na kuwezesha wanachama waliosajiliwa kwenye mfumo kufikia 21,850,” amesema.


Katika Wilaya hiyo, Makada 119 walichukua fomu kuomba kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya Chama hicho, ambapo nafasi ya Mwenyekiti waliomba makada sita, huku nafasi ya uenezi wakiomba makada watano akiwemo anayemaliza muda wake, Hussein Jamali.

Nafasi ya wajumbe wa Mkutano mkuu wa CCM Taifa, wameomba makada 38, akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Moshi Abas Kayanda na Regina Chonjo, huku Halmashauri kuu ya Wilaya wakiomba Makada 35, Mkutano mkuu wa Mkoa 17 na Halmashauri kuu ya Mkoa kupitia Wilaya makada 17.

Chanzo Mwananchi

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments