Muhimbili Kuanzisha ‘Sober House’ Vikuruti

Hospitali ya Taifa Muhimbii (MNH) imesema inatarajia kuanzisha huduma jumuishi za waraibu wa dawa za kulevya katika kijiji cha marekebisho ya afya ya akili kilichopo Vikuruti kata ya Chamazi.
Dar es Salaam. Hospitali ya Taifa Muhimbii (MNH) imesema inatarajia kuanzisha huduma jumuishi za waraibu wa dawa za kulevya katika kijiji cha marekebisho ya afya ya akili kilichopo Vikuruti kata ya Chamazi.

 Pamoja na hilo pia imepanga kuanzisha kliniki ya magonjwa ya afya ya akili eneo hilo ili kupunguza msongamano uliopo MNH-Upanga.

Wakati kukiwa na mpango huo, utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu Kishiriki cha Sayansi na Afya Muhimbili (MUHAS) mwaka 2018 kuhusu watu wanaotumia dawa za kulevya nchini ulionyesha Watanzania kati ya 200,000 hadi 450,000 wameathirika na dawa za kulevya aina ya heroin.

Utafiti huo pia ulionyesha katika jiji la Dar es Salaam pekee waraibu wa kilevi hicho wakifikia takribani watu 10,000.

Mipango hiyo imeelezwa leo Novemba 18 na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Profesa Mohamed Janabi alipofanya ziara kijijini hapo ambapo alipokea taarifa ya kijiji hicho na kuzungumza na wagonjwa na watumishi.

Profesa Janabi aliridhishwa na namna kazi za uzalishaji zinavyofanyika kijijini hapo licha ya kuwepo kwa changamoto mbalimbali ikiwemo uchakavu wa miundombinu.

"Tutashirikiana na sekta binafsi kuhakikisha tunafanya maboresho makubwa hapa ikiwemo kuzungushia uzio kwenye eneo lote la ekari 160, kujenga majengo mazuri, pamoja na kuanzisha makazi ya kisasa ya kusaidia waraibu wa dawa za kulevya (sober house) ambao watasaidiwa kitaalamu zaidi," alisema Profesa Janabi.

Awali akiwasilisha taarifa kwa Mkurugenzi Mtendaji, Mkuu wa Kijiji cha Vikuruti Beno Kalunga alisema kuwa kwa sasa kijiji kinahudumia wagonjwa 7-10 kwa mwezi, pia kinajihusisha na kilimo na ufugaji ikiwa ni sehemu ya tiba kazi kwa wagonjwa.

Alisema wagonjwa wanaohudumiwa Vikuruti ni wale waliopata changamoto za afya ya akili na kutibiwa hivyo hupelekwa kijijini hapo kwa lengo la kuendelea na tiba kazi ili afya zao ziimarike vizuri.

Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Muhimbili, Dk John Rwegasha ambaye kitengo hicho kipo chini ya kurugenzi yake alisema kuwa atahakikisha anasimamia utekelezaji wa mipango ya kuboresha kijiji hicho hatua kwa hatua.

Methadone ni dawa inayotumika kutibu utegemezi wa dawa zingine za kulevya ikiwemo heroin, cocaine, Ephedrine, Diazepam, na morphine. Dawa hii ambayo huzuia arosto na kupunguza utegemezi hutolewa kwa kipimo maalumu chini ya usimamizi wa wataalamu wa afya ya akili.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments