Waziri Nape Azungumzia Mabadiliko Bei Bando la Intaneti

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema hakutakuwa na mabadiliko ya bei za bando yoyote hadi tathmini ya gharama itakapokamilika.

Tathmini hiyo inayofanywa kila baada ya miaka mitano, inatarajiwa kukamilika kati ya Desemba 2022 hadi Januari 2023.

 Ameyasema hayo leo Jumatatu, Novemba 21, 2022 wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliofanyika makao makuu ya ofisi za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), jijini Dar es Salaam.


Nape amesema kwa sasa watoa huduma wote wako katika viwango vya bei elekezi iliyowekwa na Serikali ambayo ni kati ya Sh2.03 hadi Sh9.35.


"Hatutegemei mabadiliko yoyote kwa kipindi hiki hadi tathmini itakapokamilika, niwaombe wananchi wasione hatuhangaiki na suala hili, tumekuwa tukihangaika nalo."


"Sasa tumefikia hatua ambayo tumesema tutatulia hadi tathmini itakapokamilika na matumaini yetu kuwa itatupa muelekeo mzuri," amesema Nnauye


Hiyo ni kutokana na kile alichokieleza tathmini itaelezea uwekezaji uliofanyika, hatua za kikodi zilizochukuliwa, marekebisho yaliyofanyika na itatoa matokeo kuwa gharama zinaweza kushuka kwa kiasi gani.


"Lakini wakati tukisubiri matokeo ya tathmini hiyo hakutakuwa na mabadiliko na tumewataka TCRA kwani wanapaswa kupelekewa maombi ya mabadiliko kuwa kwa sasa watulize sekta watu waendelee kutumia huduma," amesema


Hili linafanyika ikiwa ni muendelezo wa ushughulikiaji malalamiko ya wananchi juu ya upandaji holela wa vifurushi unaofanywa na mitandao ya simu jambo ambalo limekuwa likifanya vilio kusikika kila kona.


Malalamiko hayo yamekuwa yakijikita zaidi katika bando la intaneti, kwa mfano mtandao mmoja nchini umebadilisha bei za kifurushi cha data kilichouzwa kwa Sh1,000 awali kiliwezesha megabaiti 450 kwa wiki, lakini sasa kwa bei hiyo zinapatikana megabaiti 350 sawa na upungufu wa asilimia 10.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments