CCM Kilimanjaro yawanyooshea kidole makada wake


 Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kilimanjaro, kimewaonya makada wake ambao wameanza kujipitisha majimboni na kujitangaza kama wabunge watarajiwa, kuacha mara moja, huku kikisema kitashughulika na viongozi na wanachama watakaobainika kukwamisha wabunge walioko madarakani, kutekeleza majukumu yao.

Kauli hiyo imetolewa leo, Februari 2,2023 na Katibu wa CCM, Mkoa wa Kilimanjaro, Jonathan Mabihya wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Uru Kusini Wilaya ya Moshi, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 46 tangu kuzaliwa kwa chama hicho, ambapo pia yameenda sambamba na ukaguzi wa miradi ya maendeleo na upandaji miti.

Mabihya amesema chama hicho hakina wabunge watarajiwa, na kuwataka viongozi na wanachama kuwaacha wabunge na madiwani walioko madarakani wafanye kazi kumaliza kipindi chao cha miaka mitano.
"Kuna baadhi ya maeneo watu wameanza kujipitisha na kujiita madiwani na wabunge watarajiwa, nataka niwaambie, kwenye chama cha mapinduzi hatuna diwani wala mbunge mtarajiwa, tunao wabunge na madiwani walioko madarakani," amesema.
"Waacheni wafanye kazi wamalize kipindi chao cha miaka mitano, tutakapotangaza uchaguzi ndipo mjitokeze, na Kiongozi au mwanachama yeyote atakayewakwamisha wabunge na madiwani kutekeleza majukumu yao, chama tutashughulika nao," amesema Mabihya.


Aidha Mabihya ametumia pia nafasi hiyo kuwataka wananchi kujenga tabia ya kueleza changamoto zinazowakabili kwa viongozi wa ngazi za chini kuanzia vijiji, kata na wilaya ili zitafutiwe ufumbuzi, badala ya kusubiri wafike viongozi wa juu ndipo kulalamika.


"Ndugu zangu wananchi, niombe mjenge utamaduni wa kueleza changamoto zenu kwa viongozi kuanzia kwenye vijiji na kata na ambazo zitakuwa juu ya uwezo wao wazifikishe kwa viongozi wa juu yao kwa utatuzi. Mtakapoona kuna changamoto ya utatuzi wa changamoto hizo, fikeni ofisi za chama, tupo wazi siku zote kwani tuliahidi kuwatumikia na kuondoa changamoto zenu na tupo tayari kutekekeza kwa uaminifu," amesema.


Akizungumza Diwani wa Kata ya Uru, kusini Wilihad Kitaly amesema wanaendelea na utekelezaji wa ujenzi  miradi mbalimbali ikiwemo ya miundombinu ya Elimu, barabara pamoja na afya ambapo ujenzi wa Kituo cha Afya Uru walipokea Sh800 milioni na sasa ujenzi umefikia hatua za mwisho za utekekezaji.


"Hapa tulipo tunaona ujenzi wa Kituo cha Afya Uru Kusini unaendelea, ujenzi umefikia hatua za mwisho na ifikapo Machi mwaka huu, huduma zinatarajiwa kuanza kutolewa na kukamilika kwa kituo hiki ni mafanikio makubwa kwa wananchi wa Uru Kusini na maeneo jirani," amesema.

Chanzo Mwananch

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments