Waandishi wa habari Shinyanga wanolewa kuhusu kazi za CAG

Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) imewanoa waandishi wa habari Mkoa wa Shinyanga kuwajengea uwezo wa kutafuta na kuripoti kwa usahihi taarifa za ukaguzi na udhibiti wa fedha za umma.

Wana habari hao pia watanolewa katika mbinu za kutambua aina za ripoti za ukaguzi, Sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia uendeshaji wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo yaliyofanyika mjini Shinyanga Juni 28, 2023, Msaidizi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (AAG), Anna Massanja amesema Ofisi ya CAG imeamua kutoa mafunzo hayo kwa waandishi wa habari kutokana na umuhimu na mchango wa vyombo vya habari katika usimamizi wa fedha na mali za umma.


‘’Vyombo vya habari vina mchango muhimu katika kuhabarisha umma kuhusu shughuli za Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi ikiwemo kufanya kaguzi na kusimamia fedha na rasilimali za Taifa kwa manufaa ya umma,’’ amesema Massanja

Amesema mafunzo hayo yatawawezesha waandishi wa habari kutafuta, kuchambua taarifa za ukaguzi na hatimaye kuibua masuala na hoja zitakazoongeza tija katika usimamizi, udhibiti na matumizi ya fedha za umma.

‘’Licha ya kusaidia umma kutambua kazi na umuhimu wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi, taarifa za kiuchunguzi za vyombo vya habari pia vinaweza kuibua hoja za uchunguzi maalum. Nawasihi waandishi wa habari waendelee kuandika habari za CAG,” amesema Massanja

Mkurugenzi Idara ya Sheria kutoka Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi (National Audit Office of Tanzania – NAOT), Elieshi Saidimu amewashauri na vyombo vya habari kuendelea kuandika habari zitakazosaidia kuokoa fedha za umma.

"Waandishi andike makala na uchambuzi kuhusu ripoti za ukaguzi kuwezesha wananchi kujua kazi zinayofanywa na CAG," ameshauri Elieshi


Mwenyekiti wa Clabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Shinyanga, Greyson Kakuru ameishukuru Ofisi ya CAG kwa mafunzo hayo akisema yataongeza uelewa na uwezo wa waandishi kuripoti habari zinazohusu fedha na rasilimali za Taifa kwa maendeleo na maslahi ya umma.

Akiunga mkono hoja ya Kakuru, Mkaguzi kutoka Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi, Hagai Maleko amesema ofisi ya CAG ina taarifa na nyaraka nyingi ambazo zikichambuliwa vema, waandishi watakuwa na uwezo wa kuandika habari nyingi za kusaidia jamii katika eneo la usimamizi, udhibiti na matumizi ya fedha na rasilima za umma.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini (GCU) kutoka Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi, Focus Mauki amwataka waandishi kutumia vema elimu na ujuzi wanayopata kupitia mafunzo hayo kuhabarisha jamii huku mmoja wa waandishi, Stella Paul akiishukuru Ofisi ya CAG kwa fursa hiyo akisema imemwongezea uelewa wa shughuli za ofidi hiyo.

 

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments