Rais Samia afichua kiini cha uasi, Kikwete atoa neno

 Rais Samia Suluhu Hassan amesema kushuka kwa uchumi na mzigo wa madeni kwa Serikali nyingi barani Afrika, kumezifanya zishindwe kutoa huduma muhimu kwa wananchi, hivyo kurudisha nyuma demokrasia kutokana na kutokea kwa mapinduzi.

Rais Samia alieleza hayo jana jijini Arusha wakati akifungua mkutano wa demokrasia uliowakutanisha viongozi wastaafu wa mataifa ya Afrika kujadiliana kuhusu hali ya demokrasia barani Afrika.

Viongozi wastaafu waliohudhuria ni pamoja na Rais wa zamani wa Sierra Leone, Ernest Koroma ambaye ndiyo mwenyekiti wa mkutano huo, Waziri mkuu mstaafu wa Ethiopia, Hailemariam Desaleign na mwenyeji wao, Rais mstaafu, Jakaya Kikwete.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Rais Samia alisema katika baadhi ya mataifa, Serikali zinashindwa kulinda maisha ya wananchi wake hasa wa pembezoni na kuondoa dhuluma ikiwemo tofauti za kiuchumi, jambo linaloiweka demokrasia ya Afrika kwenye majaribu.

“Kushindwa kwa Serikali kutoa huduma muhimu kumesababisha vurugu katika baadhi ya maeneo Afrika. Wanaanzisha vikundi kuzikabili mamlaka za Serikali kwa kueleza matakwa ya wananchi kwa njia ya vurugu, hapa ndiyo vinatokea vikundi vya kigaidi na maandamano," alisema Rais Samia.

Mkuu huyo wa nchi, alisema demokrasia inatakiwa kuwa njia ya kuwashirikisha wananchi katika mambo yanayohusu maisha yao na msingi wa hilo ni kuruhusu uhuru wa vyama na uhuru wa kujieleza.

Kama njia ya kulinda demokrasia hapa nchini, Rais Samia alisema wakati wa maadhimisho ya miaka 30 ya kuanzishwa kwa mfumo wa vingi vya siasa, aliamua kuja na ajenda ya 4R ambazo zinahusisha maridhiano, ustahimilivu, mabadiliko na kujenga upya.

Rais Samia aliongeza kuwa takwimu zinaonyesha kati ya nchi 54 za Afrika, nchi 25 zimewahi kukabiliwa na mapinduzi, jaribio la mapinduzi au ghasia za uharibifu tangu mwaka 2010 hadi sasa.

“Afrika ni bara halijawa salama. Miaka minane iliyopita, kumefanyika mapinduzi 21 na kuibuka kwa migogoro mipya huko Sudan na Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

"Hali mbaya zaidi ilichochewa na mlipuko wa Uviko-19 ambao ulikuwa na athari za kiuchumi kwa nchi nyingi na kwa kiasi fulani ulisabaisha vikwazo na kuahirishwa kwa chaguzi katika baadhi ya nchi," alisema Rais Samia.

Awali, Kikwete alisema migogoro ya kisiasa, vita, Uviko-19, vita vya Ukraine na Russia, vimekuwa na athari kwa mataifa ya Afrika, hivyo viongozi wana kazi kubwa ya kufanya kutafuta suluhisho kwa mazingira ya kiafrika.

Alisema kila nchi ina historia yake ya kusimulia, lakini anaweza kusema kwa kujiamini kwamba Tanzania ina bahati waasisi wake, Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Amani Karume waliweka msingi imara ambao viongozi waliofuata akiwemo yeye waliendeleza ujenzi wa Taifa.

"Sasa Tanzania ni watu milioni 61, tuna vyama vya siasa 19, lakini tunaishi kwa amani. Bado kuna changamoto tunahitaji kuendelea kuzifanyia kazi, ili kuijenga nchi yetu. Rais wetu (Rais Samia) unafanya kazi nzuri na endelea kufanya kazi kama kaulimbiu yako inavyosema 'kazi iendelee'," alisema Rais Kikwete.

Kwa upande wake, Rais mstaafu Koroma alisema kuna mambo mengi yanayoendelea Afrika ambayo yanawaacha watu na maswali mengi kuliko majibu. Alisema mambo kama vile vita vya hivi karibuni nchini Sudan, migogoro inayoendelea Somalia, Nigeria, Mali, Burkina Faso, DRC, 

Jamhuri ya Afrika ya Kati na nchi nyingine, kuenea kwa misimamo mikali, kuongezeka kwa umaskini na matatizo ya kiuchumi, kumeharibu familia na kuziacha kwenye maumivu makubwa.

Alisema kiini cha kuporomoka kwa kasi kwa demokrasia, kunaonekana kupitia taasisi za kidemokrasia kama vile Bunge na Mahakama zinazopaswa kuangalia utendaji wa Serikali, lakini mara nyingi ndiyo zinazoongoza kwa uvunjaji wa katiba na vitendo visivyo vya kidemokrasia, kama vile kutumia magonjwa ya milipuko kwa faida yao kukandamiza sheria.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments