VIJANA na Watoto wamepaza sauti zao wakieleza kwa kina changamoto zinazowakabili watoto na vijana kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi huku wakitoa rai kwa viongozi wa Bara la Afrika kuzingatia ukweli huo watakapokuwa wanajadiliana.
Hasa kuhusu changamoto za mabadiliko ya Tabianchi katika Kongamano linalofanyika nchini Kenya, na kuomba viongozi hao kuchukua hatua stahiki kukabiliana na hali hiyo.
Wakizungumza leo wakati wa majadiliano yaliyohusisha wanafunzi wa Shule za Msingi , Sekondari pamoja na Vijana katika Mkoa wa Dar es Salaam Kama yalivyoandaliwa na Jukwaa la Mabadiliko ya Tabia nchi (FORUMCC) wamesema mabadiliko ya Tabia nchi yanahatarisha afya na ustawi, lishe, elimu, maendeleo, maisha na mustakabali wa watoto na vijana.
Wamesema kwa mujibu wa Ripoti ya 6 ya IPCC (Jopo la Kimataifa Kuhusu Mabadiliko ya Tabia Nchi) inaonya kuwa bila mabadiliko makubwa ya kiuchumi na nishati na kupunguza ongezeko la joto hadi 2ºC, matukio mabaya zaidi kwa watoto yataongezeka na kuongezeka kwa kina cha bahari kunaweza kulazimisha zaidi ya watu milioni 200 kuhama, na kudumaza ukuaji wa watoto milioni 1.4 ifikapo mwaka 2050.
Kupitia taarifa yao kwa vyombo vya habari Watoto na Vijana hao wamesema Ripoti ya 6 ya IPCC inasema wazi hatari za kutochukua hatua juu ya mabadiliko ya Tabia nchi ni kubwa na kwamba njia ya kusonga mbele inahitaji mabadiliko ambayo hayajawahi kushuhudiwa.
Wameeleza kuwa masuala yenye changamoto kubwa ya ukosefu wa usawa wa kiuchumi, mamlaka ya kisiasa, na haki ya kijamii lazima yashughulikiwe na watu wa rika na jinsia zote ndiyo maana mkataba wa Paris katika sura yake ya kwanza unakubali mabadiliko kuwa mabadiliko ya Tabia nchi ni wasiwasi wa kawaida wa wanadamu, na ni wakati wa kuchukua hatua.
Wameongeza kwamba ni Vema Viongozi wa Mataifa ya Afrika wanakutaka katika kongamano nchini Kenya wakazingatia kuwa kushughulikia mabadiliko ya Tabia nchi, kunahitaji kuheshimu, kukuza na kuzingatia wajibu wao husika juu ya haki za binadamu, haki ya afya, haki za jamii za asili, serikali za mitaa, wahamiaji, watoto, watu wenye ulemavu na watu walio katika mazingira magumu wakikosa haki ya maendeleo.
"Kama usawa wa kijinsia, uwezeshaji wa wanawake na usawa kati ya vizazi ni muhimu katika muktadha huu, ni watoto na vijana wa siku hizi ambao watakabiliwa na athari mbaya zaidi za mabadiliko ya Tabia nchi.
" Utashi wa kisiasa unahitajika ili kuimarisha jitihada za kuhimili athari za mabadiliko ya Tabia nchi hususani shughuli zinazolenga mtoto ili kujenga Jamii stahamilivu dhidi ya athari hizo. Hatua za pamoja ikiwa ni pamoja na ushirikishwaji wa vijana ni muhimu.
" Watoto na Vijana, wamewakumbusha Viongozi wa Kiafrika kuzingatia maazimio Kupitia Chombo cha Umoja wa Mataifa kinachoratibu shughuli za mabadiliko ya Tabia nchi Mkataba (UNFCCC) wakati wa Mkutano wa 11 wa Wanachama (COP11) mwaka 2005 huko Montreal (Canada) uliotambua haja ya kuwashirikisha vijana katika jitihada zote za kuhimili athari za mabadiliko ya Tabia nchi, " wamesema.
Pia Watoto na Vijana wamewaomba viongozi wa Kiafrika kusisitiza jinsi ilivyo muhimu kuwashirikisha vijana na watoto katika hatua za muktadha wa mabadiliko ya Tabia nchi na kutoa wito zaidi kwa wakuu wa hao nchi za Afrika kuendelea kuwa imara na wenye umoja kwa uamuzi muhimu ambao utajenga misingi ya Haki katika kuhimili athari za mabadiliko ya Tabia nchi kama iliyoainishwa upya kwa mazingira ya Kiafrika, kwa usawa endelevu sasa na kwa vizazi vijavyo.
Wamesema wanatarajia na wanaamini matokeo ya mkutano huo kwa gharama yoyote na juhudi yanaakisi haki za watoto katika mipango mikakati na shughuli kuhusiana na mabadiliko ya mabadiliko ya Tabia nchi kwa lengo la kufikisha ndoto na matarajio ya vijana wa Kiafrika na ustawi endelevu wa watu wa Afrika.
Pia wanatambua ukweli kuwa Watoto na Vijana wanaunda vikundi vya jamii vinavyokabiliwa na athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi huku wakifafanua sababu za changamoto hiyo ni pamoja na nafasi finyu ya kushiriki katika midahalo husika, mipango na michakato ya kufanya maamuzi.
Aidha, wamesema siku chache zilizopita, madai ya wadau kutoka Asasi Zisizo za Kiserikali (AZAKI) ilitaja hali halisi ya makundi maalum na yaliyo hatarini katika muktadha wa mabadiliko ya mabadiliko ya Tabia nchi, na kuwataja vijana na watoto kuwa miongoni mwa makundi yanayohitaji kuwa mada kuu na muhimu wakati wa majadiliano ya Mkutano huo.
Hivyo wametoa wito kwa usaidizi wa kina, unaojumuisha usaidizi wa kifedha, teknolojia, na utaalam, ili kuendeleza ubunifu, uvumbuzi na ufumbuzi miongoni mwa vijana na hivyo kuongeza ushuriki wao katika kuhimili na kukabiliana na athari za mabadiliko ya Tabia nchi
Matukio mbalimbali katika picha wakati watoto na vijana mkoani Dar es Salaam wakijadili masuala mbalimbali ya mabadiliko ya tabianchi yanavyoathiri watoto na vijana.
0 Comments