Mtwara. Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Deogratius Ndejembi amewataka viongozi wa umma kuwa na akiba ya maneno hasa wanapoona vyombo vya habari.
Akizungumza na watumishi wa Mkoa wa Mtwara amesema imekuwa kawaida viongozi kutoa kauli zinazowaingiza kwenye migogoro na watumishi wenzao hali aliyosema inapoteza dhana ya utawala bora.
Amebainisha kuwa katika kipindi hiki hatarajii kuona migogoro kazini wala viongozi kuwaweka ndani watumishi na kutaka mtumishi aadhibiwe kulingana na taratibu za utumishi ikiwemo kumwagiza mkurugenzi kumuandikia barua ya onyo.
"Wapo wenye mamlaka ya kuweka watumishi ndani haya ni matumizi mabaya ya madaraka, hivi tukiamua kuwawajibisha kwa kufuata taratibu za utumishi hamuoni itasaidia sana kuliko kuwaweka ndani, jaribuni kujishusha.”
"Chukueni hatua kwa watumishi ambao wamehatarisha amani na usalama wa nchi na mtumishi akikosea asionewe hatua zichukuliwe stahiki. Mfano akutwe anafanya biashara za magendo huyo mchukulieni hatua haraka lakini kwa makosa mengine hatua za utumishi zifuatwe, ila sio umemkuta kwenye starehe usiku, asubuhi unamchukulia hatua, huu si utawala bora,” amesema.
0 Comments