WAKATI TUNABORESHA VIKOSI, TUSISAHAU NA VIWANJA VYETU PIA




 ACHA kazi iendelee kwa sasa hasa kwenye upande wa maboresho ya timu zote kuanzia Ligi Kuu Bara, Ligi Daraja la Pili, Ligi ya Wanawake kwa usajili kuendelea.

Kimbembe kinaanza kwa wachezaji wenyewe ambapo unaona kwamba kwa sasa wapo kwenye hesabu za kukamilisha madili mapya na wengine tayari kazi wameshaifunga.

Ukiwaweka kando hao wachezaji pia benchi la ufundi, viongozi nao wamekuwa bega kwa bega kutoa sapoti wakishirikiana kwenye kutimiza majukumu yao uwanjani.

Hali hii inaleta picha nzuri kule ambako tunatarajia kwenda kutokana na kila mmoja kuwa na kitu ambacho anakifikiria kwa sasa na anakitenda kwa wakati.

Wale ambao wapo Ligi Daraja la Kwanza wanajua kile ambacho wamekivuna kwani tayari Geita na Mbeya Kwanza wameshapanda na zile za kushuka zimejua fungu lao kwa msimu mpya.

Hamna namna ya kufanya kwa sasa kwa kuwa maisha lazima yaendelee na kwa kuwa kwenye ushindani ni lazima aonekane ambaye anashindwa. Lazima itatokea wapatikane wa kushuka na wale wa kupanda.

Zipo timu ambazo zinaanza maisha mapya kwenye Ligi Daraja la Kwanza ikiwa ni pamoja na Gwambina, Ihefu, Mwadui na JKT Tanzania.

Kushindwa kwa sasa haina maana kwamba wao sio bora hapana ni hesabu tu zimewagomea  wanaweza kujipanga upya wakarudi wakaendelea na kasi yao ile walipokuwa wanaanza msimu.

Zile ambazo zimepanda kwa wakati huu wa usajili ni muhimu kuwa makini na kusajili wachezaji wazuri na wenye uzoefu.Ikiwa hivyo itaongeza nguvu na ushindani pia kwenye ligi.

Kikubwa kinachohitajika ni maandalizi makini na kila mmoja kutimiza majukumu yake kwa wakati sahihi itaongeza ushindani na kuleta matokeo mazuri.

Kasumba ile ambayo imekuwa ikiwasumbua wengi kuonyesha ushindani mzunguko wa pili isipewe nafasi na badala yake ni lazima kila mmoja afanye kazi kwa ushirikiano.

Zile ambazo zimetoka kushiriki Ligi Daraja la Kwanza zina kazi kubwa ya kuanza kufanya maandalizi ili ziweze kuleta ushindani wa kweli ndani ya ligi.

Wepesi kwenye kupanda wanajua wale waliopanda lakini ugumu wa kupanda pia wanajua wale ambao wameshuka namna ambavyo wanapambania kufikia malengo yao.

Zipo timu nyingi ambazo zilishuka na zikashindwa kurudi kwenye ubora wake hii ilitokana na ushindani ambao walikutana nao kwenye Ligi Daraja la Kwanza.

 Matukio haya yawe darasa kwa timu ambazo zinapambana kupanda kwenye ligi nazo zinapaswa zijue kwamba huku juu mambo sio mepesi kama ambavyo wanafikiria.

Matumaini yangu ni kwamba kupitia matukio haya yanayoendelea wamiliki wa timu, wachezaji pamoja na wamiliki wa timu wanaona namna mambo yanavyokwenda hivyo wataongeza umakini wakati watakapokuwa kwenye ushindani.

Tunataka kuona timu ikipanda kwenye ligi iwe na uwezo na vigezo vya kuhimili mikikimikiki ya huku kwani hakuna kuzubaa ni mwendo wa kukimbizana.

Ukiachana na ligi kuu ya wanaume pia kuna ligi ya wanawake hapa pia kuna umuhimu wa kuitazama kwa ukaribu ili kutengeneza timu makini pia kwa wanawake.

Kutokana na ushindani uliopo hasa kwenye timu za wanawake kuna umuhimu wa wadau kujitokeza pia kutoa sapoti kwa wanawake ili nao pia waweze kuleta ushindani.

Kwa sasa kuna mashindano pia ya kimataifa kwa bingwa wa ligi ya Wanawake hapo ni lazima kuwe na uwekezaji pia na ushindani mkubwa.

Zawadi kubwa huku iwe kwenye kuwaboreshea mazingira yao ya kazi hasa kuanzia viwanja pamoja na vitendea kazi.

Katika hili pia iwe fundisho katika kuangalia usalama na uwepo wa wachezaji wetu kwani wanajitoa kwa ajili ya kazi kwa kufanya mchana hata usiku ila hakuna ambaye anawajali.

Kuna umuhimu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutazama namna ya kuwapiga tafu wachezaji pamoja na timu kiujumla kwani wengi hali zao bado hazijawa sawa.


Mazingira magumu ya maandalizi yanafanya timu iweze kufungwa mabao mengi kwenye mchezo mmoja hili jambo sio nzuri. Jambo la msingi ni ushindani kwa kila timu kupata matokeo chanya.

Katika hili ni muhimu kutazama namna maandalizi yalivyo pamoja na fedha ambazo zinatumika kwenye maandalizi kamili kwa timu.

Wakati tukifanya maboresho kwenye timu na uwanja ni muhimu kuukumbuka. Ubora wa mchezaji unategemea mahali ambapo atakuwa anacheza.

Tunahitaji kuona kwamba kila mchezaji anacheza kwenye uwanja mzuri na timu imara. Itasaidia pia kupunguza idadi ya wale wachezaji ambao wanashindwa kutimiza malengo yao kutokana na kuumia.

Kwa namna mambo yanavyokwenda hii haileleti afya katika maisha ya soka na ili uweze kuushinda mpira na kupata matokeo ndani ya uwanja ni lazima kupambana.

Pia kuna suala la usajili ni muhimu kwa timu zote kuangalia kwa umakini namna inavyowezekana kwa ajili ya kujenga timu. 

Hapa ni muhimu kwa kila timu kufanya usajili makini kwa ajili ya wakati ujao kwani ligi inatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa. 

Uwanja wa Azam Complex ni moja ya sehemu bora ya kuchezea hivyo ni muhimu kuweza kuutolea mfano kwa ajili ya wakati ujao kwa timu binafsi. 


TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments