Recent-Post

Tafiti za mafuta na gesi asilia kuendelea mkoani Singida, TPDC wapongezwa

MKUU wa Mkoa wa Singida, Dkt.Binilith Mahenge amewapongeza wawakilishi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kwa mkakati wao wa kutoa elimu kwa viongozi na wananchi wa mkoa huo hasa katika maeneo ambayo utafiti wa mafuta unafanyika.

Akitoa pongezi hizo leo Februari 16, 2022 ofisini kwake Dkt.Mahenge amesema, endapo tafiti ambazo wanaendelea nazo zitakuwa na matokeo chanya zitasaidia kuongeza pato la taifa kupitia uuzaji wa mafuta na gesi ambayo yameonekana katika baadhi ya maeneo ya Singida na baadhi ya mikoa ya jirani.

Aidha, amewahakikishia wataalamu hao kwamba Serikali ya mkoa itatoa ushirikiano wote utakaohitajika katika kufanikisha utafiti huo kwa kuwa miradi hiyo ikikamilika itakuwa na manufaa makubwa kwa wanachi wa mkoa huo na taifa kwa ujumla.

Awali akitoa maelezo kwa Mkuu wa Mkoa Mtaalamu wa utafiti wa mafuta na gesi, Habibu Mohamedi kutoka shirika hilo amesema, shirika linafanya utafiti katika kitalu cha Eyasi Wembere kilichopo Kaskazini – Mashariki mwa Tanzania ndani ya bonde la ufa la Afrika Mashariki.
Habibu amesema, bonde la Eyasi-Wembere ni moja ya maeneo muhimu yenye miamba tabaka yenye uwezo wa kuhifadhi mafuta na gesi asilia ambalo linapita katika mikoa mitano ya Tabora, Singida,Arusha, Simiyu na Shinyanga.

Aidha, Habibu amebainisha kwamba shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia katika kitalu hicho zilianza mwaka 2015 ambapo TPDC ilikusanya taarifa za awali za kijiofizikia zenye urefu wa kilomita 11,323 za mstari.

Kutokana na tafiti hizo Bw. Habibu alieleza kwamba kati ya mwaka 2019/2020 visima vifupi vya utafutaji wa mafuta na gesi asili vilichimbwa ili kubaini aina ya matabaka ya miamba hiyo.

Hata hivyo ameendelea kubainisha kwamba katika mwaka wa fedha wa 2021/22 shirika limepanga kufanya utafiti wa kijiokemia kwa lengo la kuangalia uwezekano kupata mafuta/gesi ambapo mikoa ya Singida, Tabora, Shinyanga, Arusha na Simiyu itafanyiwa utafiti huo.
Kwa upande wake Afisa Uhusiano wa shirika hilo, Deliani Kabwogi amefafanua kwamba, mradi huo ni muhimu kwa taifa na mkoa kwa ujumla kwa kuwa kuongeza kipato na utasaidia upatikanaji wa ajira za muda mfupi wakati wa kusafisha mikuza, kulinda mashine na vifaa vitakavyotumika kwenye utafiti, huduma za malazi na chakula.

Deliana akafafanua kwamba upatikanaji wa mafuta /gesi katika eneo hilo utawezesha nchi kuwa na uhakika wa nishati ya mafuta au gesi na kuongeza mapato kupitia mauzo ya nishati ambayo yatasidia kuchangia uboreshaji huduma za kijamii.

Post a Comment

0 Comments