Maua yaacha hasara ya mabilioni, wafanyakazi maelfu wakosa ajira

Kufungwa kwa mashamba 11 ya maua mkoani Arusha katika miaka ya hivi karibuni, kumesababisha hasara ya mabilioni na zaidi ya wafanyakazi 4,000 kukosa.

Licha ya wamiliki waliopoteza mtaji, Serikali nayo imekosa zaidi ya Sh102 bilioni za kodi na malimbikizo ya mikopo.

Uchungunzi uliofanywa na gazeti hili kwa baadhi ya wamiliki wa mashamba na wadau wa sekta hiyo, umebaini kufungwa kwa mashamba hayo kumetokana na changamoto za uendeshwaji , mazingira ya magumu ya biashara na uwekezaji, athari za janga la Uviko-19, sheria na wingi wa kodi, tozo na ushuru.

Baadhi ya wamiliki wa mashamba na wadau wa sekta hiyo, wameomba mashamba hayo yafufuliwa ili miundombinu yake isiendelee kuharibika na Serikali isaidie kulipwa kwa stahiki za wafanyakazi wake wanaodai zaidi ya Sh5 bilioni.

Mkurugenzi wa shamba la Mountmeru lililowahi kuwa bora Afrika Mashariki, Lucy Urio alikiri hali ngumu ya uendeshaji kwa sasa kwani wafanyakazi wanadai zaidi ya Sh300 milioni na kuna mikopo na kodi zaidi ya Sh25 bilioni.

“Tunaiomba Serikali kusaidia mashamba haya yasiendelee kuharibika kwani ni ngumu sana kuyarejesha katika hali yake ya awali,” alisema Lucy.

Utafiti uliofanywa na Chama cha Wakulima wa Matunda na Mbogamboga Tanzania (Taha), umebaini kuwa licha ya ajira 4,010 zilizohatarini kupotea, Serikali nayo imepoteza zaidi ya Sh102 bilioni kwenye kodi huku mapato mengine Sh84 bilioni yakikosekana.

Mtendaji Mkuu wa Taha, Dk Jacqueline Mkindi anasema sekta hiyo ilikuwa inakua kwa asilimia 11 kwa mwaka lakini janga la Uviko limeishusha mpaka asilimia saba.

Hata hivyo, Dk Jacqyeline alisema wanathamini juhudi za Serikali ili kuyaokoa mashamba hayo kutokana na umuhimu wa sekta hiyo ambayo thamani ya maua, matunda, viungo na mbogamboga yaliyouzwa kimataifa iliongezeka kutoka dola 412 milioni za Marekani mwaka 2015 hadi dola 779 milioni mwaka 2019.

Mwaka 2019, Kenya iliuza nje ya nchi maua ya dola 709 milioni, Ethiopia iliuza dola 241 milioni na kuzifanya nchi hizo ziongoze kwa usafirishaji barani Afrika huku Tanzania ikiuza maua ya dola 23 milioni.

Mdau wa kilimo cha maua, Justine Peter alisema kuna changamoto zilizochangia kufa kwa mashamba hayo zikiwamo kubwa za gharama za uendeshaji.

Peter alisema umiliki wa ardhi ya kilimo, kukosekana kwa sheria inayolinda ardhi ya kilimo na uwapo wa tozo na ushuru kunaongeza gharama za uendeshaji hivyo kupunguza ushindani wa Tanzania katika masoko ya kimataifa.

“Pia kuna gharama kubwa za usafirishaji, ufanisi mdogo wa bandari na viwanja vya ndege kuhudumia mizigo inayoharibika haraka ni tatizo pia,”alisema.

Mdau mwingine wa kilimo hicho, Neema Lyimo aliiomba Serikali kusaidia kuyafufua mashamba hayo na kufuta madeni ya kampuni husika ili kuwapa wawekezaji nafasi ya kuyaendeleza hivyo kuendeleza ajira kwa Watanzania.


Mashamba yaliyofungwa

Mashamba yaliyofungwa ni Tengeru Flowers lenye ukubwa wa ekari 114 na lililokuwa na wafanyakazi 450 likimilikiwa na Kampuni ya M/s Tengeru Flowers tangu mwaka 1963, jingine ni Mount Meru Flowers lenye ekari 39.9 lililo ajiri wafanyakazi 700 slikimilikiwa na M/s Mount Meru Flowers Limited.

Shamba jingine ni Tanzania Flowers lenye ukubwa wa ekari 115.2 ambalo liliajiri wafanyakazi 300 likiendeshwa na Kampuni ya M/s Tanzania Flowers. Pia kuna Tanzania Flowers Limited lenye ukubwa wa ekari 50 na wafanyakazi 200.Inaelezwa kuwa shamba hili lilitokana na Dolly Estate ambalo baadaye lilinunuliwa na kuunganishwa na Mount Meru Flowers, yote sasa yapo chini ya Mufilisi Kabidhi.

Jingine lililofungwa ni shamba la Arusha Blooms lenye ekari 1,486 lililokuwa na wafanyakazi 300. Baadaye liligawanywa mara mbili, lipo chini ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango.

Shamba la Tanzania Flowers la ekari 209 nalo lilikuwa na watu 1,000 kwa sasa ni mali ya Serikali chini ya katibu mkuu wa Wizara ya Fedha tangu Juni 2020. Vilevile kuna shamba la Kiliflora Limited (Nduruma Farm) lenye ukubwa wa ekari 93.5 lililokuwa na wafanyakazi 500 na sasa ni mali ya Serikali tangu Juni 2020

Kutokana na wamiliki wa mashamba hayo kushindwa kurejesha mikopo waliyoichukua Benki ya TIB na Benki Kuu Tanzania (BoT), pamoja na riba, imefika Sh102.7 bilioni.

Athari nyingine iliyojitokeza, gazeti hili limegundua ni kupungua kwa mapato ya fedha za kigeni kwa kushindwa kuuza bidhaa hizo nje ya nchi wakati Serikali ikipoteza mapato yatokanayo na kodi, ushuru na leseni takribani Sh2.06 bilioni tangu yalipofungwa.

Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Shamba la Mount Meru, Hamza Selemani ameiomba Serikali kuingilia kati kunusuru mashamba hayo kwani ajira zimepotea na bado wanadai malimbikizo ya mishahara. Katika shamba hilo pekee, alisema wanadai Sh300 milioni.

Alisema kutokana na kadhia hiyo, zaidi ya ajira 4,010 zimepotea na wategemezi wao zaidi ya 40,000 wanaishi kwa taabu lkuanzia mwaka 2012.


Serikali kuyanusuru mashamba

Akizungumza kuhusu mashamba hayo, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alisema tayari ameuagiza uongozi wa Mkoa wa Arusha kuanza kuyafufua na ikiwezekana kuyagawanya kwa vijana ili waanze kulima wakati michakato mingine inaendelea.

“Nimemuomba Mkuu wa Mkoa Arusha, John Mongella atuletee andiko la kuendeleza sehemu ya mashamba haya wakati Serikali ikiendelea na hatua nyingine,” alisema Bashe.

Kwa upande wake, Mongella alisema tayari mchakato wa kushughulia mashamba hayo ili kuhakikisha yanarudi kwenye uzalisha umeanza.

“Tunalishughlikia jambo hili kama tulivyoagizwa kuhakikisha hayaendelei kuwa mapori,” alisema Mongella.

Akiwa katika ziara mkoani Arusha hivi karibuni, Rais Samia Suluhu alipokea malalamiko ya waliokuwa wafanyakazi wa mashamba hayo na kusema Serikali inayafanyia kazi hivyo kuwataka wawe watulivu.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments