Othman aeleza mafanikio yake mwaka mmoja madarakani

 Wakati Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud akitimiza mwaka mmoja wa kushika nafasi hiyo, ameeleza mambo mbalimbali aliyoyafanya ndani ya kipindi hicho katika masuala ya kiutendaji na mwenendo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).

Akizungumza na waahriri na waandishi wa habari katika hoteli ya Golden Tulip mjini Unguja leo Machi2, 2022, Othman amesema zipo hatua mbalimbali zimefikiwa zenye kuleta matumaini. 

Katika masuala ya kiutendaji Othman amezungumzia maeneo manne yanayosimamiwa na ofisi yake ambayo ni mazingira, dawa za kulevya, ukimwi na watu wenye ulemavu ambayo kwa pamoja yameundiwa mikakati kadhaa.

Othman aliapishwa kuwa Makamu wa kwanza wa Rais Machi 2, 2021 baada ya aliyekuwa Makamu wa Kwanza Maalim Seif Sharif Hamad kufariki dunia Februari 17 mwaka huo.

Amesema baada ya uchaguzi mwaka 2020 yalitokea majeraha na kuwaacha watu wengi wakiumizwa hivyo ilibidi kuwapo mambo matatu yaliyopendekezwa kutibu majeraha hayo ambayo moja kati ya hayo limetekelezwa kwa asilimia 100 huku mawili yakiwa kwenye mchakato wa utekelezaji.

"Mambo hayo ambayo yanajulikana kwa umaarufu wa hoja tatu ni kuachiwa huru viongozi 300 wa ACT Wazalendo waliokuwa mahabusu au wameshikiliwa kwa njia nyingine," amesema Othman na kuongeza kwamba hoja hii ndio imetekelezwa kwa asilimia mia moja.

Hoja nyingine ni kufanya uchunguzi huru wa kimahakama kuhusu uvunjwaji wa haki za binadamu wakati wa uchaguzi Mkuu mwaka 2020 na kufanya mapitio na mabadiliko mfumo wa uchaguzi wa Zanzibar.

Kwa mujibu wa Othman mambo haya yanahitaji tafakuri ya kina jinsi ya kuyaendeleza na mchakato wake bado unaendelea.

Pia amesema ndani ya kipindi cha mwaka mmoja akiwa msaidizi na mshauri wa Rais, ameandaa mapendekezo ya kina kuhusu namna ya kuimarisha SUK na kuyawasilisha kwa Rais Dk Hussein Mwinyi.

Ametaja sehemu ya maeneo hayo kuwa ni pamoja na kurejesha imani na kuaminiana, kujenga utengamano wa kijamii na kuleta utengamano wa kisiasa na uhuru na ustaarabu katika kuendesha siasa.

 

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments