UN yatoa Sh4.3 trilioni kutekeleza miradi ya maendeleo

Serikali imeingia makubaliano na Umoja wa Mataifa (UN) wa kutoa Sh4.3 trilioni kusaidia shughuli za maendeleo kupitia Ushirikiano wa Mpango wa Maendeleo Endelevu wa Umoja wa Mataifa (UNSDCF).

Makubaliano hayo yalisainiwa jana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba na Mwakilishi Mkazi wa UN, Zlatan Milisic.

Akizungumza mara baada ya kutiliana saini, Tutuba alisema wamekubaliana kuwa wadau hao wataendelea kusaidia afua mbalimbali za maendeleo nchini.

Alisema maeneo ya ushirikiano yatajikita katika Mpango wa Taifa Maendeleo wa miaka mitano, huku upande wa Zanzibar ukijikita katika dira ya maendeleo ya Zanzibar.

Alisema fedha hizo zitakuwa zikitekelezwa na taasisi mbalimbali zilizo chini ya Umoja wa Mataifa ambazo ziko nchini na watakuwa wakishirikiana na wizara, taasisi, mikoa na halmashauri katika utekelezaji wa shughuli hizo.

Alisema vipaumbele vya fedha hizo vimejikita katika shughuli za kawaida ambazo Serikali watakubaliana kupitia wizara, mikoa na halmashauri.

Alisema makubaliano hayo yaliyosainiwa jana yataanza kutekelezwa katika mwaka wa fedha unaoanza Julai Mosi mwaka huu hadi Juni 30 mwaka 2027.

Maeneo yatakayonufaika ni maji, afya, elimu, shughuli za usawa wa kijinsia na kupunguza umaskini.

Alisema wamekubaliana kama kutajitokeza wadau watakaoongeza ahadi zao basi viwango vitakuwa vikibadilika na vitakuwa vikiingizwa katika bajeti za kila mwaka za wizara, mkoa au halmashauri.

Naye Milisic alisema walikutana kufanya marejeo ya mwisho kuhusu UNSDCF ambao utaongoza katika kuisaidia Tanzania katika kipindi cha miaka mitano.

Akizungumza kuhusu msaada huo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Paul Loisilie alisema uwepo wa demokrasia na usawa wa kijinsia ni miongoni mwa vigezo vinavyoangaliwa na UN.

Alisema ingawa bado kuna upungufu mdogomdogo, lakini Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imeonyesha mafanikio katika maeneo hayo, ndiyo maana UN wanatoa msaada.

 

Post a Comment

0 Comments