USAID KUISAIDIA TANZANIA SHILINGI TRILIONI 3

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akizungumza wakati wa kikao kwa njia ya mtandao na Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID), Kate Samvongsiri, jijini Dodoma. Kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Bw. Emmanuel Tutuba.


Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali Bw. Emmanuel Tutuba, akichangia jambo wakati wa kikao kwa njia ya mtandao kati ya Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), kulia, na Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID), Bi. Kate Samvongsiri, jijini Dodoma.


Viongozi wa Wizara ya Fedha na Mipango wakifuatilia kikao kwa njia ya mtandao kati ya Wizara na Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID), Bi. Kate Samvongsiri, jijini Dodoma. Kutoka kushoto ni Kamishna Msaidizi Idara ya Fedha za Nje Bw. Melckzedeck Mbise, Kamishna Idara ya Madeni Bw. Japhet Justine, Kaimu Kamishna Idara ya Sera Bw. William Mhoja na Kamishna Msaidizi Idara ya Sera Bw. Mbayani Saruni.


Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID), Bi. Kate Samvongsiri (juu kulia) pamoja na ujumbe wake, wakiwa katika Kikao na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), kwa njia ya Mtandao.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WFM- Dodoma)

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), ameliomba Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani – USAID, kuelekeza kiasi cha msaada wa dola za Marekani bilioni 1.3 sawa na zaidi ya shilingi trilioni 3 inazotaka kuipatia Tanzania kupitia Asasi za kiraia, katika kipindi cha miaka 5 ijayo, zielekezwe kwenye miradi ya kipaumbele ya Serikali ya Awamu ya Sita.

Dkt. Nchemba ametoa maombi hayo Mjini Dodoma, alipofanya mazungumzo kwa njia ya mtandao na Mkurugenzi wa Shirika la Misaada ya Kimataifa la Marekani (USAID), Bi Kate Samvongsiri.

Alilishukuru Shirika hilo kwa uamuzi wake wa kutoa kiasi hicho cha fedha kupitia Asasi za Kiraia (NGOs) katika kipindi cha miaka mitano ijayo lakini akaeleza umuhimu wa miradi iliyokusudiwa kutekelezwa na asasi hizo za kiraia kuelekezwa katika vipaumbele vya Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ikiwemo sekta za afya, elimu, kilimo, na mingineyo itakayochochea ukuaji wa uchumi.

“Tunapoandaa ushirikiano mpya na mipango mipya tunaomba mzingatie vipaumbele vya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ambayo amewekeza nguvu kubwa, sambamba na yale mnayofanya kwenye sekta ya afya, elimu, kilimo, mazingira, pamoja na sekta zingine”Alisema Dkt. Mwigulu

Dkt. Mwigulu alisema kwa sasa Mhe Rais anajenga vituo vingi vya afya na hivi karibuni ataajiri watumishi wengi wa sekta hiyo, pamoja na sekta zingine ambazo anazifanyia kazi kama sekta ya elimu na kuiomba USAID kuelekeza fedha hizo ambazo nitapitia kwenye mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs), kwenye maeneo hayo.

“Mfano, vituo vya afya vingi vimejengwa na watumishi wataajiriwa, mnaweza mkaweka nguvu kwenye vitendea kazi ambavyo bado havijakamilika ili huduma ziwe zinapatikana na lengo la Serikali pamoja na malengo mliyonayo ya kuendeleza huduma za jamii ambalo mnalo liweze kutimia” Alisema Mwigulu.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani -USAID, Bi Kate Samvongsiri, alisema kuwa wanapenda kushirikiana na Serikali ya Tanzania na watakaa pamoja na kuangalia shughuli zinazofanyika katika sekta hizo za elimu, afya, kilimo, maji pamoja na zingine na kuona namna watakavyoziwezesha.

Uhusiano kati ya Tanzania na Shirika hilo la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani USAID, limekuwa na uhusiano wa zaidi ya miaka 50, na kwamba tarehe 30 Septemba, 2016, Shirika hilo lilisaini mikataba mitatu ya msaada yenye thamani za zaidi ya dola za Marekani milioni 635.5, zilizotumika kutekeleza miradi mbalimbali ya kiuchumi na kijamii, program ambayo itafikia tamati mwezi Septemba, 2022.

Na. Eva Valerian, WFM- Dodoma

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments