Makada 19 wa Chadema waachiwa huru Mwanza


 Viongozi na wanachama 19 wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) waliokuwa wakikabiliwa na shtaka la kufanya fujo kwenye mkusanyiko wa kidini katika Kanisa Katoliki Parokia ya Kawekamo jijini Mwanza wameachiwa huru.

Washtakiwa hao wameachiwa huru leo Juni Mosi, 2022 na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza,  Bonaventure Lema baada ya upande wa mashtaka kuwasilisha hati ya kutokuwa na nia ya kuendelea na shauri hilo namba 77/2021.

Kwa mara ya kwanza makada hao walifikishwa mahakamani Agosti 19, 2021 wakidaiwa kutenda kosa hilo Agosti 15, 2021 baada ya kuhudhuria ibada ya Jumapili katika Kanisa Katoliki parokia ya Kawekamo wakiwa wamevaa sare za chama chao na fulana nyekundu zilizoandikwa Katiba Mpya.

Walioachiwa huru ni pamoja na Katibu wa Chadema Kanda ya Victoria, Zakaria Obadi, Deus Shinengo, mang’ombe Oswald, Kelvin John, Farida Gilala, John Nyamhanga, Emmanuel Mtani na Frank Nyamuga.

Wengine ni Msafiri Nteminyanda, Musa Kimweri, Gadson Jacob, Elieza Mkungu, Dionise Edward, Michael Christian, Leah Joseph, James Mayala, Yasinta Wachelele na Eudia Frank. Washtakiwa wote walikuwa wanawakilishwa na Wakili Erick Muta.

Akisoma hati ya mashtaka wakati shauri hilo lilipofikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Agosti 19, 2021, Wakili wa Serikali, Bisela Bantulaki alidai mbele ya Hakimu Mkazi Emmanuel Lukumay kuwa washtakiwa walitenda kosa hilo Agosti 15, 2021 katika Kanisa Katoliki Parokia ya Kawekamo Wilaya ya Ilemela jijini Mwanza.

Wakili Bantulaki alidai kwa pamoja, washtakiwa ambao wote walikana mashtaka dhidi yao walifanya fujo wakati ibada ya matoleo ikiendelea.

Washtakiwa wote walikuwa nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya mdhamini aliyesaini hati ya dhamana ya Sh1 milioni, barua ya utambulisho kutoka ofisi ya Serikali ya Mtaa na nakala ya kitambulisho cha mpigakura au cha Taifa.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments