Waziri Makamba Aitangazia Neema Simiyu

Waziri wa Nishati nchini Tanzania, January Makamba amesema Mkoa wa Simiyu utafunguka zaidi kiuchumi kufuatia Serikali kutelekeza mradi wa usafirishaji wa umeme wa uhakika kutoka mkoani Shinyanga.

 Makamba amesema Simiyu ni mkoa wa wenye fursa nyingi za kiuchumi ikiwemo kilimo cha pamba na alizeti, hivyo uwepo wa umeme wa uhakika utachochea zaidi maendeleo ikiwemo kuwavutia wawekezaji.

Ametoa kauli hiyo leo Jumatano Julai 13, 2022 wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na mkuu wa Mkoa wa Simiyu, David Kafulila na akiwa katika eneo litakalojengwa kituo cha kupooza umeme cha Imalilo kilichopo wilayani Bariadi mkoani Simiyu.

Kwa mujibu wa Makamba, mchakato upo katika programu ya mradi wa gridi imara unaoongeza uwezo wa umeme wa uhakika kwenye maeneo yenye changamoto za nishati hiyo.

Amesema umeme wa kilovoti 220 ni mapinduzi ndani ya mkoa wa Simiyu na utaleta mabadiliko.

"Ujenzi wa mradi huu utachukua miezi 18 na ukikamilika utakuwa na manufaa makubwa kwa mkoa wa Simiyu na kutimiza malengo ya mkoa kuendeleza shughuli za uzalishaji mali. Kwa sasa tupo katika hatua ya manunuzi na mwezi ujao mkandarasi ataanza kazi hii.

"Hii ndoto ya muda ya kuona Bariadi inakuwa na umeme wa uhakika na tutaweka historia na shughuli za kiuchumi zitaendelea kufunguka. Mkuu wa Mkoa (Kafulila) waambieni wawekezaji wasiwe na wasiwasi umeme wa uhakika utakuwepo," amesema Makamba.

Maelezo hayo yalipokelewa kwa furaha na viongozi wa mkoa wa Simiyu akiwamo Kafulila akisema ni habari njema kwa kuwa kwa muda mrefu mkoa huo unahitajia umeme wa uhakika kwa ajili ya kuendesha shughuli za kiuchumi ikiwemo kuanzisha  viwanda hasa ukizingatia wanaongoza kwa kilimo cha Pamba.

"Wananchi wanahitaji wa Simiyu wakiwemo wawekezaji wanahitaji umeme kwa ajili ya shughuli za uzalishaji mali.Tunashukuru katika bajeti ya mwaka 2022/23 Serikali imetenga fedha kwa ajili ya shughuli hii ikwemo ujenzi wa kituo cha kupoozea, umeme," amesema Kafulila.

Meneja wa miradi ya usafishaji na usambazaji wa umeme wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Frank Mashalo amesema  kituo hicho kitakuwa na matoleo mbalimbali ya kusafisha umeme katika maeneo ya viwanda, wilaya za Maswa, Meatu, Busega na Itilima na njia yake itakuwa kilomita 100.

Meneja wa Tanesco mkoani hapa, Alistidia Kashemeza amesema umeme unaongia Simiyu ni mdogo na unasafiri umbali mrefu, lakini mradi wa gridi imara ukianza kufanya kazi utakuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa mkoa huo.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments