Na John Mapepele
Wadau
wa Sekta ya Utalii nchini wametumia mkutano wao na Serikali kupitia
Wizara ya Maliasili na Utalii kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuleta mabadiliko chanya katika
kipindi kifupi cha uongozi wake, huku wakisifu kasi ya sasa ya utendaji
wa Wizara.
Wadau
hao wa utalii takribani mia sita kutoka katika vyama vyote vya wadau wa
utalii nchini wameyasema hao usiku wa kuamkia leo mei 27, 2023 katika
mkutano maalum na Wizara ya Maliasili na Utalii uliochukua zaidi ya
masaa nane na kumalizika saa sita usiku, ulioratibiwa na Wizara ya
Maliasili ambapo Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mohamed Mchengerwa
akiambatana na Katibu Mkuu Dkt Hassan Abbasi na Naibu wake Anderson
Mutatembwa ameongoza menejimenti ya Wizara na taasisi zote zilizochini
ya wizara hiyo kufanya kikao maalum na wadau hao.
Kikao
hicho ambacho Mhe. Mchengerwa ndiye Mwenyekiti kimekuwa na lengo
mahususi moja tu la kujadili changamoto mbalimbali za kisekta na
kuzipatia ufumbuzi wa kudumu ili kuboresha sekta huku watendaji
wakitakiwa kujibu hoja zote za wadau.
Akichangia
hoja katika mkutano huo, Mwenyekiti wa waongoza utalii kanda ya
kaskazini (NTSGS) Qorro Englebert amempongeza Rais Samia kwa
kutumia kipindi cha mlipuko wa ugonjwa wa uviko 19 kuwapatia mafunzo
maalum wadau wa utalii zaidi ya 1000 katika vyuo vya Serikali ambayo
amedai yamesaidia kuwaongezea ujuzi maalum katika kazi zao za kila
siku.
Ameiomba
Serikali kuwapa upendeleo maalum wanafunzi wanaomaliza mafunzo maalum
ya uaskari wa uhifadhi katika vyuo vya Serikali ili waweze kutumia
taaluma hiyo waliyoisomea badala ya kuajiri askari wasiyokuwa na
elimu ya uhifadhi.
Pia
amempongeza Mhe. Rais kwa kupunguza kodi za kutua ndege na kufafanua
kuwa baada ya punguzo hilo kumekuwa na matokeo chanya ya wimbi kubwa
la ndege kuwaleta watalii.
Aidha
wadau hao wamepongeza uongozi mpya kwa kuonesha kasi mpya ya
ufanyaji kazi huku wakisifu namna Waziri Mchengerwa anavyoshirikiana na
watendaji wake katika shughuli mbalimbali huku wakifafanua kuwa
ushirikishwaji baina ya watendaji wa Wizara na wadau ni nguzo muhimu
katika kuleta mafanikio ya haraka kwenye sekta.
“Naomba
niwe mkweli Timu ya sasa hivi haijawahi kutokea. Katika kipindi kifupi
tangu kuteuliwa kwenu tumeshuhudia Mhe. Waziri na Katibu Mkuu mmekuwa
pamoja katika utendaji wenu wa kazi jambo ambalo limetupatia moyo,
kwa kasi na ushirikishwaji huu na jinsi ambayo mmeanza vizuri
tunatarajia mtatufikisha mbali.” Amesisitiza Mwenyeki Wile Chambulo
ambaye ni Mwenyekiti wa TATO nchini.
Awali
akifungua mkutano huo, Waziri Mchengerwa amesisitiza kuwa katika
kipindi hiki Serikali itakuwa karibu na wadau kwenye kila hatua ili
kuhakikisha sekta inasonga mbele kwa maslahi ya wadau na taifa kwa
ujumla.
“Kwa
kushikiana na wadau na Serikali mtegemee maboresho makubwa
yanakuja, na kamati yetu nataka ifanye kazi na ije na mapendekezo ili
marekebisho haya yaweze kufanyika haraka.” Amesisitiza Mhe. Mchengerwa
Pia
amesema katika kipindi hiki Serikali itaboresha miundo mbinu ikiwa ni
pamoja na kuweka barabara za kiwango cha lami itakayokuwa inapitika
mwaka mzima pamoja, pia kuimarisha ulinzi kwa mgeni.
Akifafanua
mchango wa sekta ya utalii amesema Sekta hii ni miongoni mwa sekta
muhimu na yenye mchango mkubwa katika kuchangia ukuaji wa uchumi wetu,
kutoa fursa za ajira na kuchochea ukuaji wa sekta nyingine muhimu.
“Mathalan,
katika kipindi cha kuanzia mwaka 2021 hadi mwaka 2022 mchango wa sekta
hii ulikuwa takribani asilimia 17 ya pato la Taifa, ambapo idadi ya
watalii iliendelea kuongezeka kutoka watalii 922,692 mwaka 2021 hadi
kufikia watalii 1,454,920 kwa mwaka 2022. Mapato yatokanayo na utalii
yaliongezeka kutoka kutoka Dola za Marekani Bilioni 1.3 mwaka 2021 hadi
kufikia Dola za Marekani Bilioni 2.5 mwaka 2022. Kadhalika, sekta hii
ilitoa fursa za ajira takribani milioni 1.5 za moja kwa moja na zisizo
za moja kwa moja." Ameongeza Mhe Mchengerwa
Amesema
mafanikio hayo yanatokana na jitihada kubwa zinazofanywa na Mheshimiwa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuipa kipaumbele sekta hii
kupitia uwekezaji wa aina mbalimbali alioufanya pamoja na ushirikiano
imara uliopo baina ya sekta za umma na Sekta Binafsi.
0 Comments