Rais Samia mgeni rasmi siku ya mashujaa

Rais Samia Suluhu Hassan kesho anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa yatakayofanyika katika uwanja mpya uliopo Mtumba jijini Dodoma.

Waziri Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Jenista Mhagama amesema hayo katika taarifa iliyotolewa na kitengo cha mawasiliano kwa umma cha wizara hiyo leo Jumatatu Julai 24, 2023.

“Shughuli za maadhimisho hayo ni pamoja na gwaride la maombolezo, uwekaji wa silaha za asili na maua kwenye mnara wa mashujaa pamoja na dua/sala kutoka kwa viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini nchini,”amesema Mhagama.


Pia amesema Rais ataweka jiwe la msingi la ujenzi wa uwanja mpya wa kumbukumbu za mashujaa.

Amesema katika kukuza uzalendo kwa wananchi, maadhimisho ya mwaka huu yatafanyika katika mikoa na wilaya zote hapa nchini kwa kufanya shughuli za kijamii kama vile kupanda miti.

Shughuli nyingine ni kufanya usafi maeneo ya kijamii na kufanya kumbukumbu ya mashujaa kwa mikoa na wilaya ambayo ina minara au makaburi ya mashujaa.

Mhagama amewahamasisha wakazi wa Mkoa wa Dodoma kufika mapema kuanzia Saa 12 asubuhi kesho kwenye kumbukumbu hizo muhimu kwa historia ya nchi.

Pia amewataka kuendelea kuwa wazalendo na kutunza tunu za nchi za amani na utulivu.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments