Recent-Post

Shungu: Kwa huyu Maxi subirini muone!

KAMA wewe shabiki wa timu pinzani na Yanga, kisha ulishangilia kitendo cha straika Fiston Mayele kutimka katika kikosi hicho, basi sikia maneno ya kushtua kutoka kwa kocha mmoja mkongwe akimzungumzia winga mpya wa mabingwa hao, Maxi Nzengeli.

Maxi ni kati ya wachezaji wanane waliosajiliwa na Yanga kwenye dirisha la usajili litakalofungwa Agosti 31 na nyota huyo kutoka AS Maniema Union ya DR Congo tayari ameanza kuwasha moto tangu kwenye siku ya Kilele cha Wiki ya Mwananchi.

Hata hivyo, Kocha Raoul Shungu aliyewahi kuinoa Yanga na sasa yupo AS Vita, alisema mashabiki waendelee kutulia kwani kazi atakayoifanya Maxi ni kubwa kiasi wanaweza hata kumsahau, Mayele aliyetua Pyramids ya Misri.


Kocha Shungu aliliambia Mwanaspoti, kama kuna usajili wa maana Yanga wameufanya basi ni kumchukua Maxi akidai winga huyo ni toleo jipya badala ya lile la Fiston Mayele.

Shungu ambaye ni kocha mkongwe wa zamani wa Yanga alisema Maxi ni mchezaji mwenye kiwango kikubwa, aliyekuwa amebaki katika Ligi Kuu ya DR Congo na kwamba kipaji chake haitakuwa rahisi kushikika hapa nchini.

Shungu alisema kama ambavyo alisema kuhusu Mayele kipindi anasajiliwa kuwa atasumbua nchini, vilevile anatoa tahadhari kwa timu pinzani kwa Yanga kumchunga Maxi kwa kuwa kipaji cha winga huyo na umri wake vitamfanya awe staa mkubwa hapa.

“Niliona Yanga ilimsajili Maxi, watu wa hapa Tanzania waelewe huyu ni mchezaji mwingine bora kabisa amekuja hapa, naweza kusema kama ni kitabu basi Maxi ni toleo jipya badala ya Fiston (Mayele),” alisema Shungu anayetamani kikosi chake kicheze na Yanga ikiwa ni siku chache tangu itoke kucheza na Singida Fountain Gate na kulala 2-1.

“Unakumbuka nilikwambia kuhusu Fiston wakati ule anafika hapa tena kabla ya kuanza kucheza? Nilikwambia ni mchezaji bora ambaye kama ataweka juhudi atasumbua sana na ikawa hivyo, nafikiri mliona wote sasa vilevile timu pinzani zimchunge huyu Maxi,” alisema Shungu aliyeiongoza Yanga kwenye makundi ya Ligi ya Mabingwa mwaka 1998 na kuongeza;.


“Kipaji chake ni kikubwa sana anaweza kucheza nafasi nyingi uwanjani, ana nguvu, kasi na kitu kizuri zaidi kwa Yanga watafaidi kwa kuwa ni kijana mdogo atawasaidia sana mtamuona pia akifunga sana.”

Shungu alisema bahati kubwa ambayo Yanga waliipata kwa kumpata Maxi kirahisi ni kutokana na ligi ya kwao Congo kusimama ambapo haikumpa nafasi kubwa winga huyo kung’aa.

“Yanga walibahatika sana, ligi yetu iliposimama nadhani ndio sababu iliyowarahishia kumpata, vinginevyo angekuwa na ofa nyingine kubwa kushinda ya hapa, nafikiri Yanga walikuwa wanamfuatilia kabla ya hapo ndio maana wakamfuata haraka,” alisema Shungu na kuongeza;

“Niliwahi kusema mtu anayewaonyesha Yanga wachezaji bora wa Congo wanatakiwa kumtunza, sijaona akiwapotosha amekuwa akiwapa wachezaji bora, watu wa Yanga watamfurahia sana (Maxi).”

Mbali na Maxi, Yanga pia imewasajili, Hafiz Konkoni, Pacome Zouzoua, Skudu, Gift Fred, Jonas Mkude, Nickson Kibabage na Yao Kouassi, waliochukua nafasi za Mayele, Bernard Morrison, Dickson Ambundo, David Brayson, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Erick Johola, Tuisila Kisinda, Yannick Bangala, Feisal Salum na Djuma Shaban.

Post a Comment

0 Comments